AFCON 2013; Cote D'Ivoire yaingia robo fainali
27 Januari 2013Siku ya nane ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika iifanyika huko Rustenburg, ambako Tembo wa Cote D'Ivoire wakitokea kutoka katika kuonyesha mchezo dhaifu wakati wa michezo ya ufunguzi na kuonyesha ubabe wake dhidi ya Tunisia kwa kuibamiza mabao 3-0, magoli yakifungwa na Gervinho, mchezaji mwenzake katika ligi ya Uingereza Yaya Toure , na pia mchezaji wa akiba aliyeingia dakika za mwisho Didier Ya Konan.
Wakati Togo ilipoishangaza mabingwa wa zamani wa kombe hilo Algeria kwa kuichapa mabao 2-0 katika mchezo wa pili, Cote D'Ivoire walihakikishiwa nafasi ya kwanza katika kundi D, bila kujali matokeo ambayo yatatokea wakati pazia litakapofungwa katika duru ya kwanza ya ligi hiyo ndogo Jumatano wiki ijayo katika kundi hilo.
Togo , ambayo ilijipatia mabao yake kupitia mshambuliaji wa Tottenham Hot Spurs Emmanuel Adebayor na mchezaji wa akiba Dove Wome, ilipata ushindi wa kushtua dhidi ya Algeria , na sasa inahitaji tu sare dhidi ya Tunisia kuweza kuchukua nafasi ya pili katika kundi hilo na kutinga katika robo fainali.
Algeria na Tunisia vichwa chini
Wakati timu hizo mbili zikisherehekea kazi nzuri walizofanya, hali ilikuwa ya fadhaa katika kambi ya Algeria , timu yenye wachezaji wenye vipaji lakini hawana uzoefu.
Kocha Vahid Halilhodzic aliwasili katika mkutano wa kawaida wa baada ya mchezo na waandishi habari akionekana kuwa katika hali ya masikitiko makubwa , kama vile mtu aliyeshinda fedha nyingi katika bahati nasibu, lakini akagundua kuwa mbwa amekula tikiti yake iliyoshinda.
"Ni maafa makubwa, " amesema.
"Najihisi aibu kubwa. Sijui kile kilichotokea leo, ni vigumu kufanya tathmini.
"Pengine wachezaji hawajakuwa wapevu vya kutosha kushiriki katika kiwango hiki.
"Lakini sitamshutumu yeyote, nilifanya uchaguzi. Ninajihisi tu aibu.
"Hali yangu ya baadaye kama kocha haina umuhimu, kile chenye umuhimu ni kwamba tunajaribu kuangalia juu ya vipi tunaweza kucheza kiwango kile cha mchezo na kisha tunashindwa.
Ameongeza: "Inaeleweka mashabiki wamekasirika, walikuwa na matarajio makubwa."
Togo, ambayo ilibakiza dakika mbili tu kuweza kuidhibiti Cote D'Ivoire katika mchezo wao wa ufunguzi, ilifanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza katika mashindano haya ya kombe la mataifa ya Afrika tangu pale walipoweza kuishinda Cameroon miaka 13 iliyopita.
Adebayor ambaye alikubali kujiunga na timu hiyo baada ya mvutano wa muda mrefu juu ya malipo ya bonasi , usalama na hali ya soka nchini Togo, alionekana mwenye furaha wakati alipojitokeza mbele ya waandishi habari.
"Tulicheza vizuri dhidi ya Cote D'Ivoire , lakini kwa bahati mbaya , hatukushinda. Tumekuja pamoja na kusonga mbele na hii inaonesha kuwa iwapo kila mtu atajiunga pamoja tunaweza kupata mafanikio makubwa."
Kocha Didier Six hakutafuna maneno: "Tulipambana na timu nzuri sana ya Algeria, tulistahili kushinda. Togo ilikuwa na nia ya ushindi."
Adebayor ambaye alijificha chini ya kiti cha basi wakati timu yao iliposhambuliwa kwa risasi kabla ya fainali za mwaka 2010 nchini Angola na watu wawili wakafariki, aliongeza: "Ni muhimu kila wakati kufunga katika fainali za kombe la Afrika. Tulijua kuwa tunahitaji kushinda baada ya kushindwa katika mchezo wa kwanza. Tulishambulia vizuri, na kutumia nafasi zetu tulizozipata. Na sasa natumai kutakuwa na sababu nyingi za kufurahi.
Drogba apumzishwa
Hapo mapema , kocha wa Cote D'Ivoire Sabri Lamouchi alitoa kali, kwa kumuacha nje nahodha Didier Drogba wakati akizungusha kikosi chake kutoa nafasi kwa wengine.
Duru ya mwisho
Wakati duru ya mwisho ya michezo ya makundi ya kombe la mataifa ya Afrika ikianza leo Jumapili (27.01.2013) kwa michezo ya kundi A, timu kadha bado zinanafasi ya kufuzu kuingia katika duru ya robo fainali, katika fainali hizi za 29 za michuano ya bara ka Afrika.
Kundi A linaongozwa na Afrika kusini , Bafana Bafana , wakati wenyeji hao wa mashindano wakiwa na points 4, Morocco na Cape Verde zikiwa na points mbili kila moja na Angola ikiwa na point moja.
Iwapo Afrika kusini itaishinda Morocco mjini Durban , timu ngeni katika mashindano haya Cape Verde itahitajika kupata sare tu dhidi ya Angola kujihakikishia kusonga mbele.
Iwapo Bafana Bafana itatoka sare na simba hao wa milima ya Atlas Morocco, Cape Verde inaweza kuchukua uongozi wa kundi hilo ikiwa itapata ushindi dhidi ya Paa weusi wa Angola, ambao wenyewe wanaweza pia kuingia katika duru ya robo fainali iwapo watawapa kipigo "papa wa buluu" , Cape Verde, na kuwafungasha virago Morocco na Cape Verde.
Mambo yanaweza kuwa katika hali ya utata zaidi iwapo Afrika Kusini Bafana Bafana itashindwa dhidi ya Morocco, nani anaweza kuwa na uhakika wa kuingia katika robo fainali ni ushindi tu wa Cape Verde utakaoweza kuizuwia Bafana Bafana.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae/afpe
Mhariri : Grace Patricia Kabogo