Baerbock na mwenzie wa Ufaransa wakutana na viongozi Syria
3 Januari 2025Matangazo
Ziara ya wanadiplomasia hao ni ya kwanza kufanywa na wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya, tangu Bashar al-Assad alipoondolewa madarakani mwezi Desemba. Baerbock amesema ziara hiyo inayofanyika kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, inapeleka ujumbe wa wazi kwa Wasyria kwamba mwanzo mpya wa kisiasa kati ya Ulaya na Syria, na kati ya Ujerumani na Syria unawezakana. Barrot amesema Ufaransa na Ujerumani kwa pamoja zinasimama na watu wa Syria. Wanadiplomasia hao pia wamelitembelea gereza maarufu la Sednaya, karibu na Damascus, kama ishara ya utawala wa kikatili wa Assad.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema Ujerumani ina mawasiliano ya karibu na waliochukua madaraka Syria na makundi ya upinzani ya Syria.