Bayern Munich yafuzu nusu fainali Champions League
11 Aprili 2013Goli la kwanza la Bayern Munich limepachikwa kimiani na Mario Mandzukic katika dakika ya 64, huku Claudio Pizarro akiifungia timu hiyo bao lake la pili dakika ya 90. Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali, Bayern Munich iliifunga Juventus mabao mawili kwa bila nyumbani na hivyo kuifanya timu hiyo kuwa na jumla ya magoli manne kwa bila dhidi ya Juventus.
Nahodha wa Bayern Munich, Philipp Lahm amekiambia kituo kimoja cha televisheni nchini Ujerumani kuwa hamasa ya mashabiki ndio iliamsha morali kwa wachezaji, ingawa walikabiliwa na wakati mgumu katika dakika 15 za mwanzo za mchezo huo. Lahm amesema timu bora nne za Ulaya zimeingia nusu fainali, huku Ujerumani ikiwa na timu mbili, hivyo hawana budi kulifurahia jambo hilo.
Dalili nzuri kwa Bayern Munich
Bayern Munich ambayo mwishoni mwa juma lililopita wameshinda taji la 23 la ligi ya Soka nchini Ujerumani-Bundesliga na kuweka rekodi kuwa washindi wa mapema katika ligi hiyo, zikiwa zimesalia mechi sita kwa msimu kukamilika, pia imefanikiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani.
Katika mechi nyingine iliyochezwa nchini Uhispania, timu ya Barcelona imefuzu kuingia hatua ya nusu fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, baada ya kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na Paris St. Germain-PSG.
Mechi hiyo imechezwa huku kocha wa Barcelona, Tito Vilanova, akiamua kumuweka mchezaji wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi kama mchezaji wa akiba hadi katika dakika ya 62, baada ya mchezaji wa PSG, Javier Pastore kuifungia timu yake bao. Messi aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Cesc Fabregas. Katika dakika ya 71, Pedro akasawazisha goli la PSG na kuwapa matumaini Barcelona ya kusonga mbele.
Kocha wa PSG aipongeza timu yake
Hata hivyo, kocha wa PSG, Carlo Ancelotti, amesema uwezo wa timu yake katika michuano hii umeipa msingi imara timu hiyo ambao utajengeka katika jaribio jingine la kushinda kwa mara ya kwanza taji hilo la Ulaya kwenye msimu ujao. Katika mchezo wa mwanzo wiki iliyopita Barcelona na PSG zilitoka sare kwa kufungana mabao mawili kwa mawili.
Ama kwa upande wa mechi nyingine za robo fainali zilizochezwa Jumanne usiku, Borussia Dortmund ilifanikiwa kuingia nusu fainali baada ya kuifunga Malaga mabao matatu kwa mawili. Nao Real Madrid walifuzu kuingia katika nusu fainali, japokuwa walishindwa katika mchuano wa mchezo wao ugenini dhidi ya Galatasaray.
Real walifungwa magoli matatu kwa mawili, lakini wamefuzu kuingia nusu fainali kutokana na jumla ya magoli matano, yakiwemo matatu ya mchezo wa kwanza. Mechi za mwanzo za nusu fainali zitachezwa tarehe 23 na 24 ya mwezi huu wa Aprili, huku fainali za michuano hiyo, ikichezwa Mei 25 mwaka huu, katika uwanja wa Wembley.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,DW
Mhariri: Iddi Ssessanga