Bundesliga kulipishwa gharama za usalama wakati wa mechi
14 Januari 2025Mnamo mwaka 2014, mji wa bandari wa Bremen ulipitisha sheria inayotoza DFL gharama za ziada kwa ulinzi wa polisi unaotolewa wakati wa mechi kali za Bundesliga na matukio mengine makubwa ya kibiashara yanayokusanya zaidi ya watu 5,000, yanayojulikana kuwa na uwezekano wa kuzuka vurugu. Mechi hizo zimeainishwa kuwa hatari pale ambapo vurugu kati ya mashabiki wa timu pinzani zinatarajiwa.
Mnamo 2015, DFL ilipokea hundi ya kwanza kutoka Bremen yenye thamani ya euro 400,000 kwa gharama za polisi wa ziada kwenye mechi ya Bundesliga kati ya Werder Bremenna Hamburg. Tangu wakati huo, Bremen imeendelea kutoza DFL kwa gharama zaidi za polisi, naWerder Bremen iko katika hali ngumu ya kifedha hadi sasa inadai jumla ya euro milioni 3.
DFL ilikata rufaa mahakamani, ikipinga uhalali wa sheria hiyo kwa hoja kuwa usalama wa umma ni jukumu la msingi la serikali za majimbo, na kwamba malipo hayo yalikiuka sheria. Hata hivyo, mahakama ya juu imeamua kuwa sheria ya Bremen inaambatana na katiba ya Ujerumani. Rais wa mahakama hiyo, Stephan Harbarth, alieleza kuwa lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha gharama zinabebwa na wale wanaofaidika moja kwa moja na tukio hilo.
Soma pia:Schalke waangukia pua tena
Kwa upande wake, DFL imejitetea kwa kusema kuwa ni watu binafsi wanaosababisha vurugu, si vilabu vya kandanda, na kwamba jiji la Bremen halikutoa maelezo ya wazi juu ya jinsi gharama hizo zilivyokokotolewa, kama inavyotakiwa na katiba.
Uamuzi wa Mahakama
Hapo awali, mnamo 2017, mahakama ya chini ya Bremen ilikubaliana na hoja ya DFL, ikisema kuwa jiji hilo halikuwa limeeleza kwa uwazi jinsi lilivyokokotoa gharama za ziada za ulinzi zilizotozwa. Hata hivyo, uamuzi huo ulibatilishwa baadaye kupitia rufaa. Mahakama ya juu ya utawala ya mjini Leipzig ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ndogo ya Bremen, na sasa Mahakama ya Katiba imeidhinisha kuwa sheria hiyo ni halali.
Baada ya uamuzi huu, inasubiriwa kuona iwapo miji mingine ya Ujerumani itaiga mfano wa Bremen na kuanza kutoza vilabu vya Bundesliga gharama za ziada za ulinzi.
Wasimamizi wa kandanda wameonya kuwa hatua hii inaweza kuongeza mzigo mkubwa wa kifedha kwa vilabu vya kandanda na kusababisha tofauti za kisera katika majimbo mbalimbali, hali ambayo inaweza kuathiri usawa wa ushindani kwenye ligi.