China, Misri zaelezea wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Syria
13 Desemba 2024Nchi hizo zimetoa tahadhari kwamba makundi ya kigaidi na yenye itikadi kali yanapaswa kuzuiwa kuzusha machafuko eneo hilo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alipokuwa akimpokea mjini Beijing mwenzake wa Misri Badr Abdelatty.
"Pande zote mbili zimeonyesha wasiwasi mkubwa juu ya hali ya sasa nchini Syria. Tunatoa wito wa kuheshimiwa mamlaka, uhuru na mipaka ya Syria, pamoja na kuanzishwa haraka iwezekanavyo kwa mchakato shirikishi wa kisiasa na kuzuia makundi ya kigaidi na yale ya itikadi kali kutumia fursa ya hali ilivyo ili kuzusha machafuko."
Katika hatua nyingine, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amemueleza rais wa Uturuki Tayyip Erdogan walipokutana jana mjini Ankara kwamba raia wa Syria wanapaswa kulindwa. Kauli hii inajiri baada ya Uturuki kusema haitalegeza msimamo wake katika vita dhidi ya magaidi nchini Syria baada ya kupinduliwa kwa rais Bashar al-Assad.