Jeshi la Israel lamshikilia mkurugenzi wa hospitali Gaza
28 Desemba 2024Matangazo
Taarifa ya wizara ya afya inayodhibitiwa na kundi la Hamas imeeleza kuwa "vikosi vya Israel vimewachukua makumi ya wahudumu kutoka Hospitali ya Kamal Adwan na kwenda nao kizuizini kwa mahojiano, akiwemo mkurugenzi, Hossam Abu Safiyeh." Kadhalika shirika la ulinzi wa raia wa Gaza liliripoti kuwa Abu Safiyeh yupo kizuzini, na kuongeza kuwa mkurugenzi wa shirika hilo kwa kaskazini, Ahmed Hassan al-Kahlout, ni miongoni mwa wanaoshikiliwa. Jana Ijumaa, jeshi la Israel lilifanya operesheni katika eneo la Hospitali ya Kamal Adwan, kwa madai kuwa kituo hicho ni "ngome muhimu ya makundi ya kigaidi", kauli ambayo imekanushwa na Hamas.