Kesi ya Bashir yaahirishwa kutokana na corona
21 Julai 2020Watu wengi walikuwa wamekusanyika katika mahakama ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, mapema leo asubuhi ambako Bashir mwenye tabasamu usoni, mwenye afya nzuri alikuwa amepandishwa kizimbani akiwa amevalia vazi refu la utamaduni wa Wasudan la Jalabiyya.
Jaji wa mahakama hiyo amesema kutokana na watu kujaa sana katika chumba cha mahakama, hali ambayo hairuhusu uzingatiaji wa umbali unaotakiwa wa watu kutokaribiana kwa mujibu wa hatua za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, kesi dhidi ya Bashir imeahirishwa na itasikilizwa tena Agosti 11 mwaka huu.
Al Moaz Hadra mmoja wa mawakili waliowasilisha keshi hiyo mahakamani ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba Bashir anakabiliwa na mashitaka ya kuiendea kinyume katiba, kuvunja sheria kuhusu majeshi na uasi.
Wakili Hadra aidha amesema, "Kesi hii ni onyo kwa mtu yeyote, awe anatokea katika ulingo wa siasa au jeshini, anayejaribu kuharibu mfumo wa katiba. Hiki ni kitendo cha kihalifu kwa mujibu wa sheria. Tutalinda demokrasia ya Sudan kupitia kesi hizi."
Mawakili wasema kesi imechochewa kisiasa
Hashem al-Gali, mmoja wa mawakili 150 wa upande wa utetezi amelalamika kuhusu kesi dhidi ya Bashir akisema ni mchezo mchafu wa siasa unaofanywa.
"Hii ni kesi ya kisiasa ambayo inaendeshwa kwa kisingizio cha sheria kama kesi halali. Ni kesi ya kisiasa inayofanyika katika mazingira ya ukatili kwa upande wa mfumo wa mahakama na upande wa utetezi."
Wakili Hashem al Gali aidha amesema keshi dhidi ya Bashir inalilenga vuguvu la kiislamu na lengo lake kubwa ni kulionyesha vuguvugu hilo kama la kigaidi.
Bashir, mwenye umri wa miaka 76 atapandishwa kizimbani pamoja na washitakiwa wengine kadhaa, wakiwemo mamakamu wawili wa rais wa zamani pamoja na mawaziri na magavana wa zamani.
Iwapo atatiwa hatiani Bashir, ambaye tayari anatumikia kifungo kwa ufisadi, huenda akakabiliwa na hukumu ya kifo.
Al Bashir aliingia madarakani mnamo mwaka 1989 baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya waziri mkuu aliyechaguliwa kwa njia ya demokrasia Sadek al-Mahdi. Aliondolewa mnamo Aprili 2019 kufuatia migomo na maandamano ya barabarani ya kudai demokrasia.
(afp)