Majaji wajiunga na maandamano Sudan
24 Aprili 2019Taarifa kutoka kwa kundi la majaji inasema majaji hao wanatarajiwa kuanza maandamano yao nje ya makahama ya katiba hadi katika makao makuu ya kijeshi, kuunga mkono mabadiliko yanayotakikana ya kuwa na mahakama zenye uhuru.
Wakati hayo yakiarifiwa viongozi wa maandamano hayo wametishia kuandaa maandamano ya taifa zima iwapo watawala wa kijeshi hawatoridhia matakwa yao ya kurejesha utawala wa kiraia.
Hata hivyo baraza hilo la kijeshi linaloshikilia madaraka limesema limewaalika viongozi wa maandamano kwa mazungumzo katika ikulu ya rais hii leo jioni. Awali wakati wa mkutano na waandishi habari kiongozi mkuu wa upinzani alisema viongozi wa maandamano wanatarajiwa kukutana ana kwa ana na Mkuu wa Baraza la kijeshi Abdel Fattah al-Burhan.
"Tuko tayari kuzungumza na jenerali Burhan na nadhani masuala yetu yatatatuliwa kupitia majadiliano," alisema kiongozi huyo wa upinzani Omar el-Digeir alipokuwa akizungumza na waandishi habari.
Al sisi na wenzake wataka Jeshi la Sudan kupewa muda zaidi kukabidhi madaraka
Jumapili iliyopita viongozi wa maandamano ya kutaka mabadiliko ya kidemokrasia na kisiasa nchini humo walisema wameyaahirisha mazungumzo yao na baraza la kijeshi baada ya kudai kuwa linaendeleza matakwa ya serikali iliyopita iliyoongozwa na rais aliyepinduliwa madarakani mnamo Aprili 11 Omar Hassan al Bashir.
Jeshi lilimuondoa al-Bashir madarakani baada ya miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya utawala wake wa kiimla. Maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakipiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, wakitaka viongozi wapya wa kijeshi kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.
Waandamanaji hao wamepata uungwaji mkono kutoka Marekani inayotaka pia jeshi likabidhi mara moja madaraka kwa serikali ya kiraia. Lakini hapo jana viongozi wa kiafrika waliokusanyika nchini Misri katika mkutano ulioitishwa na rais Abdel Fattah al-Sisi, walilisisitiza haja ya Sudan kupewa muda zaidi wa miezi mitatu kwa jeshi hilo kukabidhi madaraka.
Hata hivyo Umoja wa Afrika mnamo Aprili 15 ulitishia kuiondoa sudan katika Umoja huo iwapo itashindwa kukabidhi madaraka hayo ndani ya muda wa siku 15.