1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiondoa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwaiathiri Kongo

Caro Robi/Philipp Sandner8 Desemba 2011

Huku Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ikisubiri kutangazwa kwa matokeo kamili ya uchaguzi wa urais leo (08.12.2011) jioni baada ya kucheleweshwa kwa siku mbili, maswali yanaibuka kuhusu wajibu wa jumuiya ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/13Oeu
Wapiga kura wakilalamikia kuchelewa kwa upigaji kura nchini Kongo.
Wapiga kura wakilalamikia kuchelewa kwa upigaji kura nchini Kongo.Picha: AP

Uchaguzi wa Kongo uliofanywa tarehe 28 Novemba umekumbwa na hali tete tangu mwanzo wa shughuli hiyo, wakati vituo vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa, vingine kukosa vifaa vya kupigia kura na mashambulio ya waasi dhidi ya maafisa wa usalama na wapiga kura katika maeneo kadhaa nchini humo.

Tume ya uchaguzi nchini humo (CENI) ilitoa matokeo ya awali Jumamosi iliyopita yaliyopuuzwa na upinzani na ambao ulionya kuwa huenda kukazuka ghasia endapo Tume hiyo haitaheshimu uamuzi wa raia wa Kongo.

Matokeo ya awali yalipaswa kutangazwa Jumanne wiki hii, lakini yakaahirishwa hadi leo jioni na hivyo kuongeza joto la kisiasa nchini humo. Jumuiya ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, imetoa wito kwa wanasiasa wa pande zote husika kudumisha amani na kuonyesha ukomavu katika kipindi hiki.

Lakini jamii ya kimataifa imechangia vipi katika kuhakikisha shughuli hiyo ya uchaguzi mkuu inaendeshwa kwa amani na kwa utaratibu unaohitajika? Claudia Simons ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa ya Afrika ya Kati anasema mifumo ya kisiasa katika mataifa ya kati yanachochea mshindi wa chaguzi kujilimbikizia madaraka yote bila ya kushirikisha upande wa upinzani.

"Wasiwasi katika chaguzi za Afrika ya Kati unatokana na mifumo ya kisiasa inayomfanya mshindi kuchukuwa yote na anayeshindwa kukosa kila kitu. Hayo yanasababishwa na kwamba mwenye mamlaka ndiye pia mwenye nguvu za kiuchumi." Amesema Bi Simons.

Wapiga kura wakilalamikia wizi wa kura nchini Kongo.
Wapiga kura wakilalamikia wizi wa kura nchini Kongo.Picha: AP

Uchaguzi wa kipindi hiki nchini Kongo, ambao ni wa pili baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ndio wa kwanza ambapo jamii ya kimataifa ilijiondoa katika kuufadhili na hivyo kuilazimu serikali kusimamia bajeti kubwa ya kuendesha zoezi hilo. Huenda hili limechangia pakubwa kwa matatizo ya kiufundi yaliyoshuhudiwa katika uchagzi huo.

Simons anasema jamii ya kimataifa ina mchango mkubwa katika ufanisi wa chaguzi hasa katika nchi ambayo mwaka 2006 ilipata uungwaji mkono kifedha na pia kiusalama kutoka mataifa mengi ya kigeni na umoja wa mataifa.

"Ingawa jumuiya ya mataifa haina uwezo mkubwa, lakini inaonekana kuwa baada ya uchaguzi wa 2006 maendeleo ya Kongo hayakupewa tena kipaumbele. Ni jambo la kawaida tu: Baada ya uchaguzi huru wa kwanza kufanyika jumuiya ya mataifa inaanza kujiondoa." Amesema Simons.

Wachambuzi wengine wanasema kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado itahitaji usaidizi mkubwa katika kuimarisha siasa za kidemokrasia kutoka jamii ya kimataifa.

"Ingawa mambo yote hayakuendeka vizuri, lakini hata hivyo inabidi mataifa ysaidie katika ile ambayo bado ni mchakato wa kidemokrasia. Yakosoe serikali na yasimamie asasi za kiraia." Amesema Alex Veit mtaalamu wa masuala ya kitamaduni ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bremen, Ujerumani:

Kufikia sasa, Rais aliyepo madarakani, Joseph Kabila, anaongoza dhidi ya mpinzani wake, Etienne Tshikedi, huku matokeo kamili yakisubiriwa kwa hamu kubwa nchini humo.

Mwandishi: Caro Robi/Philipp Sandner
Mhariri: Mohammed Khelef