1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni Siku ya Wakimbizi duniani

Caro Robi
20 Juni 2017

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ametoa wito wa ushirikiano zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa katika kuushughulikia mzozo wa wakimbizi duniani. 

https://p.dw.com/p/2ezXa
Kongo Flüchtlinge
Picha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Gabriel amesema Ujerumani haiwezi pekee yake kukabiliana na changamoto na hivyo inahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na jukumu la kushughulikia wakimbizi kusambazwa kwa usawa ili kupunguza mateso wanayokumbana nayo wakimbizi kote duniani na kuzuia mzozo wa muda mrefu wa wakimbizi.

Ujerumani imesema imeongeza mara kumi bajeti yake ya kutoa misaada ya kiutu katika nchi za kigeni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ili kuwalinda wakimbizi katika nchi wanazotokea kwa mfano Syria.

Ujerumani yataka mzigo wa wakimbizi kusambazwa

Ujerumani imewapokea zaidi ya wakimbizi milioni moja wanaotoroka vita na mizozo kutoka Mashariki ya kati na Afrika katika miaka ya hivi karibuni. Sigmar amesema mwaka jana ilitumia euro bilioni 1.3 kutoa misaada, na hivyo kuifanya Ujerumani kuwa mojawapo ya nchi karimu zaidi katika suala la matumizi ya kibinadamu.

Südsudan Flüchtlinge
Wakimbizi wa Sudan Kusini walioko UgandaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Umoja wa Mataifa hapo jana ulisema ghasia, mizozo na mateso Syria, Sudan Kusini na kwingineko yamewaacha watu milioni 65.5 duniani bila ya makazi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, hiyo ikiwa ongezeko la watu laki tatu ikilinganishwa na mwaka 2015.

Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi amesema idadi hiyo ndiyo kubwa kuliko zote tangu waanze kuchukua takwimu za wakimbizi duniani ,akiongeza idadi hiyo haipaswi kukubalika kwani inaonyesha haja ya kuungana na kuwa na mtizamo mmoja katika kuepusha mizozo.

Inakadiriwa kila baada ya sekunde tatu kuna mtu ambaye anayahama makazi yake.

Machafuko ya Sudan Kusini yamekuwa chanzo cha mzozo wa dunia unaokuwa kwa haraka unaochangia kwa watu kutoroka makaazi yao. Idadi ya Wasudan Kusini waliotorokea nchi nyengine iliongezeka kwa asilimia 64 na kufikia milioni 1.4 katika nusu ya pili ya mwaka jana.

Idadi kamili kwa sasa imefikia karibu milioni 1.9 huku watu wengine milioni 2 wakiwa wakimbizi ndani ya nchi yao Mkuu wa UNHCR barani Afrika Valentin Tapsoba amesema, hakuna mzozo wa wakimbizi unaomtia wasiwasi duniani sasa hivi kama ule wa Sudan Kusini.

Wanawake na Watoto wakimbizi ndiyo waathiriwa wakubwa

Zaidi ya wakimbizi elfu mbili wanaingia Uganda kutokea Sudan Kusini kila siku tangu ghasia kuzuka upya mwezi Julai mwaka jana. Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia watoto, nusu ya idadi hiyo ni watoto, wanaowasili wakiwa wagonjwa, wamechoka na walio na matatizo ya kisaikolojia.

UNHCR Südsudan Flüchtlinge
Wanawake wakimbizi na watoto katika kambi ya AdjumaniPicha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Uganda inawahifadhi wakimbizi milioni 1.1. Zaidi ya watoto wakimbizi laki tano kutoka Sudan Kusini, zaidi ya wakimbizi 134,000 kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na zaidi ya 27,000 kutoka Burundi. Msytica Achieng afisa wa UNICEF Uganda amesema wanawake na watoto kutoka Sudan Kusini, Congo na Burundi wanahitaji kwa dharura huduma za afya, maji safi, elimu na zaidi msaada wa kisaikolojia.

Siku ya Alhamisi na Ijumma wiki hii, Uganda itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kujadili masuala ya kuwapa ulinzi wakimbizi na wahamiaji. Mzozo wa Syria peke yake ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 6 sasa, umewafanya watu milioni 5.5 kutafuta usalama katika nchi nyingine, ikiwemo zaidi ya watu 800,000 mwaka jana pekee, jambo linaloifanya nchi hiyo kuwa inayotoa wakimbizi wengi duniani.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga