1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aapa kusalia madarakani baada ya serikali kuporomoka

6 Desemba 2024

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amelihutubia taifa kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Michel Barnier, ambaye aliondolewa madarakani baada ya bunge kumpigia kura ya kihistoria ya kutokuwa na imani naye.

https://p.dw.com/p/4nomU
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.Picha: Ludovic Marin/AFP

"Mnamo tarehe 9 Juni, nilitangaza kulivunja bunge. Kwangu, uamuzi huo ulikuwa hauepukiki. Kwanza, kwa kuwa uchaguzi wa bunge la Ulaya ulikiweka chama cha Rassemblement National na kuwaweka wenye siasa kali mbele. Pili, viongozi wengi wa kisiasa walikuwa wanatabiri kura ya kutokuwa na imani kwenye majira haya ya mapukutiko. Hata hivyo, ninapaswa kukiri kwamba uamuzi huu haukufahamika. Wengi wamenikosoa, na najuwa wengi wanaendelea kufanya hivyo. Huo ni ukweli na hii ni dhamana yangu." 

Ndivyo alivyosema Rais Macron jioni ya jana wakati akikubali kwamba kuporomoka kwa serikali ya Waziri Mkuu Michel Barnier kulitokana na maamuzi yake mwenyewe Macron wakati akijaribu kurekebisha mambo yaliyokwishakwenda kombo. 

Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Ufaransa awasilisha barua ya kujiuzulu

Katika hotuba yake hiyo kwa taifa, Macron alitupilia mbali wito wa kujiuzulu unaotolewa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani na badala yake kuashiria kwamba atabakia hadi mwisho wa muhula wake mwaka 2027.

Waziri Mkuu mpya kuteuliwa

Hata hivyo, Macron aliahidi kwamba atamteuwa waziri mkuu mpya siku za hivi karibuni, ili kuizuwia Ufaransa isitumbukie kwenye mpasuko zaidi wa kisiasa baada ya kuanguka kwa serikali ya Barnier.

Waziri Mkuu wa Ufaransa aliyeondolewa na bunge, Michel Barnier.
Waziri Mkuu wa Ufaransa aliyeondolewa na bunge, Michel Barnier.Picha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

"Ndiyo maana nitamteuwa waziri mkuu mpya siku za karibuni. Nitamuomba kuunda serikali kwa maslahi ya umma, inayowakilisha kila nguvu ya kisiasa miongoni mwa vyama vilivyopewa dhama ya kuongoza na ambavyo vinaweza kujiunga na serikali, ama angalau, kukubaliana na sio kuiporomowa. Waziri Mkuu mpya atashauriana na kuunda serikali yenye ufanisi zaidi kwa ajili yenu. Kipaumbele chake kikubwa kitakuwa bajeti." Alisema Macron ambaye, hata hivyo, hakutaja siku ya kumtangaza waziri mkuu huyo.

Soma zaidi: Barnier atarajiwa kujiuzulu kama waziri mkuu wa Ufaransa

Macron aliwakosowa vikali wabunge wa mrengo mkali wa kushoto na kulia kwa kile alichodai kuwa kuungana kwao dhidi ya serikali ya waziri mkuu ni kinyume na maslahi ya umma wa Ufaransa.

Ofisi ya rais ilikuwa imesema mapema kwamba Barnier na mawaziri wake wataendelea kwenye nyadhifa zao hadi hapo serikali mpya itakapoteuliwa.