1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mawaziri wa EU wasaini vikwazo vipya dhidi ya Russia

16 Desemba 2024

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wamesaini vikwazo vipya dhidi ya Russia. Vikwazo hivyo ni vya 15 tangu Russia ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022.

https://p.dw.com/p/4oCqd
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya waonyesha mshikamano wao na Ukraine katika vita vyake dhidi ya uvamizi wa Russia
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya waonyesha mshikamano wao na Ukraine katika vita vyake dhidi ya uvamizi wa RussiaPicha: Francois Lenoir/European Union

Hayo yakijiri rais wa Urusi Vladimir Putin amesema wanajeshi wake wako na uwezo mkubwa katika uwanja wa mapambano dhidi ya Ukraine. 

Vikwazo vipya vya kiuchumi, vinalenga kuizuia Urusi kuepuka vile ambavyo tayari vipo vilivyowekwa na umoja huo, na pia vinalenga kudhoofisha uwezo wa jeshi na viwanda vyake vya ulinzi.

Meli 52 ziliongezwa kwenye orodha ya meli ambazo zinashukiwa kutumiwa na Urusi. Aidha vikwazo hivyo pia vimelenga kampuni 32.

Watu 84 wamewekewa marufuku ya usafiri na mali ya mashirika kadhaa pia yanakusudiwa kuzuiwa, kufuatia matendo yao yanayohujumu uhuru wa Ukraine.

Unaweza kusoma pia: Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine

Kupitishwa rasmi kwa vikwazo vipya na mawaziri wa mambo ya nje waliokusanyika Brussels dhidi ya Urusi, kunafuata makubaliano yaliyofikiwa wiki iliyopita na mabalozi wa Umoja wa Ulaya.

Akizungumza na waandishi habari alipowasili kwenye mkutano huo, waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Bernard Quintin amesema: "Tunaiunga mkono Ukraine kikamilifu katika vita vyake dhidi ya uvamizi wa Urusi. Na kwa siku zijazo msimamo wetu unabaki vile vile. "Hakuna chochote kuhusu Ukraine, bila Ukraine." Na lazima ibaki hivyo."

Ukraine yahimiza muendelezo wa shinikizo kwa Russia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha aliyehutubia mkutano huo kwa njia ya video, aliwarai wenzake wa Umoja wa Ulaya kuendelea kuishinikiza Urusi, huku akisisitiza umuhimu wa vikwazo vipya.

Unaweza kusoma pia: Serbia yamuahidi Putin kwamba kamwe haitaigeuzia mgongo

Katika tukio jingine rais wa Urusi Vladimir Putin amesema vikosi vyake vina uwezo zaidi katika uwanja wa mapambano kote dhidi ya Ukraine.

Rais wa Russia Vladimir Putin na mkuu wake wa majeshi Vallery Gerasimov wakiteta
Rais wa Russia Vladimir Putin na mkuu wake wa majeshi Vallery Gerasimov wakitetaPicha: POOL/Grigiry Sysoyev/AFP/Getty Images

Putin amesema jeshi la Urusi limeweza kukamata makaazi 189 ya Ukraine mwaka huu wa 2024 huku akiutaja kuwa mwaka wa mafanikio makubwa katika kile anachokiita "operesheni maalum ya kijeshi" dhidi ya Ukraine.

Unaweza kusoma pia: Mashambulizi ya Urusi yawaacha watu milioni bila umeme

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Andrei Belousov aliyezungumza katika mkutano huo huo alisema katika mwaka 2024, vikosi vya Urusi vimekamata eneo lenye ukubwa wa 4, 500 kilomita mraba la Ukraine na kwa sasa, vinakamata takriban kilomita mraba 30 kila siku.

Russia yadai kuendelea kudhibiti maeneo zaidi ya Donetsk, Kherson na Zaporizhzhia

Kwa mujibu wa Belousov, Ukraine inadhibiti chini ya asilimia moja ya jimbo la mashariki Lugansk, na kati ya asilimia 25-30 ya majimbo ya Donetsk, Kherson na Zaporizhzhia.

Unaweza kusoma pia: Kremlin: Putin yuko tayari kuzungumza na Trump kuhusu Ukraine

Hayo yakijiri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte anatarajiwa kufanya mazungumzo na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, pamoja na viongozi kadhaa wa Ulaya siku ya Jumatano. Jumuiya hiyo imesema mkutano huo utafanyika Brussels Ubelgiji, mnamo wakati inajaribu kujiimarisha kabla Donald Trump kuchukua mamlaka nchini Marekani.

Viongozi wa Ulaya wamesema miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, Donald Tusk wa Poland na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.

(dpae, afpe, aptn)