Mawaziri wa Kigeni wa Ujerumani, Ufaransa waizuru Syria
3 Januari 2025Mawaziri hao, ambao waliwasili mjini Damascus kwa nyakati tafauti asubuhi ya leo, wanatazamiwa pia kukutana na wawakilishi wa asasi za kijamii na kulitembelea gereza linalofahamika kwa viwango vya kutisha vya ukatili la Sednaya, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara zao.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani iliyotolewa muda mfupi kabla Waziri Annalena Baerbock hajaondoka Berlin kuelekea Damascus, Waziri huyo ameitaja ziara yake ya leo kuwa ishara ya wazi wa watu wa Syria.
Soma zaidi: Watawala wapya wa Syria wafanya mazungumzo nchini Saudia
"Mwanzo mpya wa kisiasa kati ya Ulaya na Syria, kati ya Ujerumani na Syria." Iliongeza taarifa hiyo.
Baerbock na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, ni mawaziri wa kwanza kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya kuitembelea Syria tangu wanamgambo kuingia mjini Damascus mnamo tarehe 8 Disemba na kumlazimisha Rais Bashar al-Assad kukimbia nchi baada ya miaka zaidi ya 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, hatua iliyohitimisha miongo kadhaa ya utawala wa kidikteta wa familia ya Assad katika taifa hilo muhimu kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati.
Ufaransa yataka amani na utulivu
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, alielezea kile alichokiita matumaini ya Syria yenye mamlaka kamili, na yenye utulivu na amani.
Aliyasema hayo wakati alipowasili mjini Damascus na kuutembelea ubalozi wa nchi yake ambao ulikuwa umefungwa tangu mwaka 2012.
Soma zaidi: Vikosi vya Syria vyaanzisha operesheni Homs
Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia, Barriot alikutana na wafanyakazi wa ubalozi huo wa Kisyria ambao walikuwa wakiendelea kulishughulikia jengo la ubalozi na akasisitiza "umuhimu wa Ufaransa kurejesha mahusiano ya kibalozi kwa kuzingatia hali ya kiusalama na kisiasa."
Tangu walipouondowa utawala wa Assad, utawala mpya unaoongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) umekuwa ukifanya juhudi ya kuyahakikishia mataifa ya Kiarabu na jumuiya ya kimataifa kwamba utatawala kwa niaba ya Wasyria wote na kwamba hautakuwa sababu ya machafuko kwa mataifa mengine.
Mataifa ya Magharibi yasaka ukuruba?
Mataifa ya Magharibi yameanza kidogo kidogo kujongeleana na mkuu wa utawala huo mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, na kundi la HTS, ambalo liliwahi kuwa sehemu ya mtandao wa Al-Qaida na kundi lijiilato Dola la Kiislamu (IS).
Tayari yameanza majadiliano ya ikiwa yaliondowe kundi hilo kutoka kwenye orodha ya makundi yanayoyaita ya kigaidi.
Soma zaidi: Sura mpya ya Syria: Ujumbe wazuru Saudi Arabia, waandamanaji Douma wadai haki
Baerbock alisema licha ya kuwa na matumaini ya wazi kwa watawala wapya, lakini ni matendo yao ndiyo yatakayoamuwa.
"Tunajuwa ilipotokea HTS kiitikadi, na kile walichokifanya. Lakini pia tunasikia na kuona hamu ya kubadilika na kufahamiana na makundi mengine muhimu," alisema akirejelea mazungumzo na kundi la waasi wa Kikurdi nchini Syria (SDF), ambao wanaungwa mkono na Marekani.