1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Medvedev: Urusi imesajili wanajeshi 280,000 tangu Januari

3 Septemba 2023

Rais wa zamani wa Urusi na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Dmitry Medvedev amesema leo kuwa, Moscow imewaandikisha takribani watu 280,000 kujiunga na jeshi la nchi hiyo tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4Vtuv
Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev
Rais wa zamani wa Urusi Dmitry MedvedevPicha: Yekaterina Shtukina/Sputnik Government/AP/dpa/picture alliance

Akizungumza wakati wa ziara yake katika kisiwa cha Sakhalin kilicho mashariki mwa Urusi, Medvedev amesema sehemu ya waliojiandikisha ni kutoka katika jeshi la akiba, wengine ni watu wa kujitolea na kutoka katika makundi mengine.

Soma zaidi: Rais wa zamani wa Urusi asema jeshi la nchi hiyo litaingia Kiev na Lviv

Dmitry Medvedev aliyeiongoza Urusi tangu mwaka 2008 hadi 2012 amekuwa sauti muhimu katika kumuunga mkono Rais Vladimir Putin kwa hatua yake ya uvamizi dhidi ya Ukraine.

Tangu mwanzoni majira ya machipuko, jeshi la Urusi limeendesha kampeni ya kusajili wanajeshi wa kujitolea kwa kufanya matangazo mengi mitandaoni na katika mitaa nchini humo.