1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Merz aahidi kuisaidia Ukraine katika vita dhidi ya Urusi

Angela Mdungu
9 Desemba 2024

Mgombea wa Ukansela anayepewa nafasi kubwa katika uchaguzi ujao wa Ujerumani Friedrich Merz ameahidi kuisaidia Ukraine na kuikosoa sera ya sasa ya Ujerumani inayoifanya Ukraine ipambane katika mazingira magumu.

https://p.dw.com/p/4nw4d
Ukraine Kyjiw 2024 | Präsident Selenskyj empfängt CDU-Vorsitzenden Merz
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Mwenyekiti wa Chama cha CDU Friedrich MerzPicha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mjini Kyiv na Rais Volodymyr Zelensky, Merz  anayeunga mkono kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu ya Taurus , amesema anataka jeshi la Ukraine liwe na uwezo wa kushambulia kambi za jeshi zilizoko ndani ya Urusi. Amesema hawalengi kuwashambulia wananchi, wala miundo mbinu ya kiraia bali kambi zinazotumiwa na Urusi kuishambulia Ukraine.

Kansela Scholz tofauti na Merz amekuwa akikataa ombi la Zelensky la kuipa nchi yake makombora ya Taurus, akisema yatachochea zaidi mzozo wa Ukraine na kuitumbukiza Ujerumani moja kwa moja kwenye mzozo huo.

Soma zaidi: Merz awasili Ukraine kwa mazungumzo

Kwa upande wake  Zelensky amesisitiza umuhimu wa Ulaya kuwa na dhamira ya dhati ya kuihakikishia usalama nchi yake katika mazungumzo yoyote ya usuluhishi yanayolenga kusitisha uvamizi wa Urusi.

Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Remko de Waal /ANP/IMAGO

Katika hatua nyingine, Baraza la Umoja wa Ulaya limesema kuwa litaipa Ukraine dola za kimarekani bilioni 4.4. Uamuzi huo umefikiwa baada ya mataifa wanachama kuidhinisha mpango wa kuipa fedha hizo.

Msaada wa Umoja wa Ulaya umetangazwa wakati waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov akisema leo kuwa amefanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani Lloyd Austin kuhusu mkutano ujao wa Ramstein kuhusu Ukraine unaohusisha mataifa wanachama wa NATO, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zinazoiunga mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Shambulio la bomu lililotegwa kwenye gari laua mtu mmoja Donesk

Tukisalia katika mzozo huo, bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari katika mji wa Donesk unaodhibitiwa na Urusi limemuuwa mtu mmoja, na mwingine amejeruhiwa.

Ukraine
Wahudumu wa uokoaji wakijaribu kuuzima moto baada ya moja ya mashambulizi ya Urusi nchini UkrainePicha: UKRAINIAN EMERGENCY SERVICE/HANDOUT/AFP

Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutoka Urusi zinadai kuwa mtu aliyeuwawa kwenye shambulio hilo ni mkurugenzi wa zamani wa gereza la Olenivka Sergei Yevsyukov, na aliyejeruhiwa anatajwa kuwa ni mke wake.

Mnamo Julai 2022, zaidi ya wafungwa 50 wa Ukraine waliuwawa katika gereza hilo na Ukraine iliituhumu Urusi kwa kuwauwa wafungwa kwa makusudi wakati Moscow ilidai kwamba Ukraine ndiyo iliyofanya mauaji hayo kwa shambulio la roketi.