Ndege ya abiria ya Azerbaijan ilidunguliwa na Urusi: Vyanzo
26 Desemba 2024Vyanzo vinne vinavyofuatilia uchunguzi wa mkasa huo vimeliambia hayo shirika la habari la Reuters. Ndege hiyo ya abiria aina ya Embraer ilianguka karibu na mji wa Aktau nchini Kazakhstan, na kuwauwa abiria 38 kati ya 67 waliokuwemo, ndani baada ya kugeuka katika eneo la Urusi ambalo Moscow ilitumia mifumo ya ulinzi wa anga dhidi ya mashambulizi ya droni ya Ukraine katika miezi ya karibuni.
Soma pia:Azerbaijan inawaomboleza waathirika wa mkasa wa ndege
Urusi imetahadharisha dhidi ya kuenezwa uvumi kuhusu mkasa huo. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari kuwa ni muhimu kusubiri matokeo ya uchunguzi. Azerbaijan ilifanya maombolezo ya kitaifa leo kufuatia mkasa huo.
Bendera nchini Azerbaijan zinapepea nusu mlingoti, huku matukio yote ya kitamaduni yaliyopangwa leo katika kumbi za sinema na za muziki yakifutwa. Miili ya abiria waliokufa na wahudumu wa ndege hiyo inasafirishwa hadi Azerbaijan kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na shirika hilo la ndege na Wizara ya Masuala ya Dharura ya Azerbaijan.