Netanyahu: Majeshi ya Israel kusalia Mlima Hermon
18 Desemba 2024Jana Jumanne, Netanyahu alilitembelea eneo hilo na kufanya mazungumzo na maafisa wa usalama pamoja na makamanda wa jeshi.
"Niko hapa kwenye kilele cha Mlima Hermon pamoja na Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi, Kanali wa Kamandi ya Kaskazini, mkuu wa Shin Bet, na makamanda wakuu. Tuko hapa katika wakati muhimu kuamua juu ya utayari wa Israel mahali hapa muhimu hadi pale mpango mwingine utakapofikiwa unaohakikisha usalama wa Israel," alisema Netanyahu.
Israel ilichukua udhibiti wa eneo la kusini mwa Syria kwenye mpaka na eneo la mlima Golan siku chache baada ya Rais Bashar Al-Assad kuondolewa madarakani na waasi.
Maafisa wameeleza hatua hiyo kuwa ya muda tu ili kuhakikisha usalama wa mipaka ya Israel lakini hawajatoa dalili yoyote ya muda ambao wanajeshi hao watasalia.
Wiki iliyopita, waziri wa ulinzi Israel Katz aliagiza wanajeshi kujiandaa kubaki kwenye eneo la mlima Hermon katika msimu wa baridi.