Papa Francis azungumzia tena "ukatili" wa Israel huko Gaza
22 Desemba 2024Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelaani kwa mara nyingine tena mashambulio ya Israeli kwenye Ukanda wa Gaza na kuyaita kuwa ni ya ukatili licha ya Israel kumshutumu kiongozi huyo kuwa kile ilichosema ni ''ndumilakuwili''.
Akiwa katika sala ya mwishoni mwa juma, Papa Francis amezungumzia jinsi mashambulizi hayo yanavyosababisha maafa na kusema anaona uchungu kuona watoto wakishambuliwa kwa risasi na mabomu katika shule na hospitali katika ukanda wa Gaza.
Soma zaidi. Papa Francis azungumzia "ukatili" unaotendeka Gaza
Siku ya Ijumaa Papa Francis akitoa hotuba katika makao makuu ya kanisa katoliki duniani mjini Vatican, kiongozi huyo wa kiroho alisema kile kinachoendelea Gaza ni "ukatili na siyo vita"
Zaidi ya Wapalestina 45,000 wameuawa katika kampeni ya kulipiza kisasi ya kijeshi ya Israel katika ardhi ya Palestina, wengi wao wakiwa raia, kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas.