Raia wa Namibia washiriki uchaguzi wa Rais
27 Novemba 2024Miongoni mwa waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa leo katika mji mkuu Windhoek ni makamu wa Rais na mgombea wa chama tawala cha SWAPO Netumbo Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72. Kama ataibuka mshindi, Nandi-Ndaitwah atakuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini humo.
Chama chake kimelitawala taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa miaka 34 tangu kilipoliongoza kupata uhuru mwaka 1990. Mpinzani mkubwa wa makamu huyo wa rais katika uchaguzi huu ni Panduleni Itula wa chama cha upinzani cha Independent Patriots for Change IPC. Mwaka 2019 Itula mwenye miaka 62 alipata asilimia 29 ya kura kama mgombea huru.
Soma zaidi: Namibia yapiga kura huku chama tawala kikikabiliwa na kinyang'anyiro kikali
Mgombea huyo amesema ana imani chama chake kitafanya vizuri kwenye uchaguzi huo. Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Namibia, karibu watu milioni 1.4 wameandikishwa kupiga kura katika taifa hilo lenye watu milioni tatu.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2019 uungwaji mkono wa chama tawala cha SWAPO ulishuka kwa asilimia 56 kutoka asilimia 87 za mwaka 2014. Ili kuchaguliwa kuwa Rais, mgombea anapaswa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura, vinginevyo kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi.
Rais wa mpito anayetetea kiti chake hagombei Urais
Kwa sasa, Namibia inaongozwa na rais wa mpito Nangolo Mbumba aliyeingia madarakani mwezi Novemba baada ya kifo cha Rais wa zamani Hage Geingob. Mbumba hagombei katika uchaguzi huu. Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa baada ya siku mbili.
Taifa la Namibia limekuwa ikishuhudia kukua kwa uchumi katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na uwekezaji katika mafuta, gesi ya hydrogen ya kijani. Licha ya hilo, nchi hiyo inashika nafasi ya pili kwa ukosefu wa usawa katika kipato, kwa mujibu wa takwimu za benki ya dunia.
Wataalamu wanabashiri chama tawala cha SWAPO kupata wingi wa kura za bunge licha ya kukabiliwa na ukosoaji kutokana na uchumi dhaifu, uhaba wa wawekezaji katika sekta ya afya pamoja na tatizo la rushwa.