1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Senegal Kupunguza Muda wa Mhula

18 Machi 2015

Rais wa Senegal, Macky Sall amesema ananuia kuitisha kura ya maoni, kuhusu kupunguzwa kwa mhula wa rais wa nchi hiyo kutoka miaka saba hadi mitano, kama mfano kwa waafrika wenzake kutong'ang'ania madarakani.

https://p.dw.com/p/1EsVT
Rais Macky Sall wa Senegal anayeazimia kuonyesha mfano wa kutong'ang'ania madarakani Afrika
Rais Macky Sall wa Senegal anayeazimia kuonyesha mfano wa kutong'ang'ania madarakani AfrikaPicha: AP

Rais Sall aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dakar, akisema watu wanapaswa kujua kwamba Afrika pia inaweza kutoa mfano, kudhihirisha kwamba madaraka ya uongozi sio kila kitu.

Sall ambaye alikuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa mtangulizi wake, Abdoulaye Wade, alisema huenda kura hiyo ya maoni kutaka kupunguza muda wa mhula wa rais kutoka miaka saba hadi mitano ikafanyika mwezi Mei mwaka ujao wa 2016. Zamani mhula huo ulikuwa miaka 5 kama ilivyo katika mataifa mengi jirani ya Afrika Magharibi, lakini ulirefushwa na rais Abdoulaye Wade.

Wakati wa kampeni yake ya uchaguzi mwaka 2012, rais Macky Sall aliahidi kuwa angeufupisha tena mhula huo kuwa miaka mitano tena, na ikiwa kura hiyo ya maoni itaridhia pendekezo lake, uchaguzi mwingine wa rais wa Senegal utafanyika mwaka 2017 badala ya mwaka 2019.

Kwingineko Afrika viongozi wajichimbia Ikulu

Haya rais Sall ameyatangaza wakati raia watatu wa nchi yake wakiwa wanashikiliwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako walikamatwa katika mkutano uliolenga kuwahamasisha vijana wa nchi hiyo ya maziwa makuu kuwa na mchango mkubwa katika siasa za nchi zao. Kwa ujumla watu 40 walitiwa mbaroni katika mkutano huo, wakiwemo raia wa nchi za magharibi ambao baadaye waliachiwa huru.

Wananchi wa Burkina Faso wakisherehekea baada ya kumfungisha virago rais Compaore
Wananchi wa Burkina Faso wakisherehekea baada ya kumfungisha virago rais CompaorePicha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Sall amesema atafanya juhudi kuhakikisha raia hao wa Senegal wanaachiwa, bila hata hivyo kujiingiza katika siasa za Kongo.

''Tumetekeleza wajibu wetu kama serikali, ambao ni kuwalinda raia wetu. Ninaazimia kuzungumza na rais Kabila ikiwa njia ya mawasiliano itakuwa imewekwa, lakini sio wajibu wangu kutoa hukumu juu ya iwapo kinachoendelea kule ni sahihi au sio sahihi. Msimamo wangu kama rais wa Senegal ni kutojiingiza katika masuala hayo'', amesema rais Sall.

Kueneza vuguvugu

Raia hao wa Senegal waliokamatwa mjini Kinshasa ni kutoka vuguvugu liitwali Y'na Marre, maana yake ''Tumechoka'', ambalo liliongoza upinzani wa kumuondoa Abdoulaye Wade Madarakani alipotaka kugombea mhula wa tatu kinyume na katiba.

Rais wa DRC Joseph Kabila ni miongoni mwa viongozi wanaoripotiwa kutaka kubadilisha katiba za nchi zao
Rais wa DRC Joseph Kabila ni miongoni mwa viongozi wanaoripotiwa kutaka kubadilisha katiba za nchi zaoPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Wao pamoja na wenzao kutoka Burkina Faso chini ya Vugu vugu liitwalo ''Ufagio wa Umma'' ambalo lilimtimua rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Blaise Compaore, walikuwa mjini Kinshasa katika mkutano ambao walisema ulikuwa na azma ya kuwahamasisha vijana wa nchi hiyo kuhusu uongozi bora na demokrasia.

Haya yanafanyika wakati Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na viongozi wa mataifa mengine katika ukanda huo, wakiwemo Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunziza wa Burundi, Denis Sassou Nguesso wa Kongo Brazzaville, na Thomas Boni Yayi wa Benin, wakiripotiwa kuwa na mipango ya kuzibadilisha katiba zao ili waweze kubakia madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo