Sall asema ushindi wake ni mwamko mpya Senegal
26 Machi 2012Televisheni ya serikali imearifu kwamba Rais Wade alimpigia simu mapema Sall na kumpongeza kwa ushindi, baada ya matokeo ya awali kuonyesha kwamba Sall ameshinda kwa kura 30,000 wakati Wade amepata kura 11,000.
Sall, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Rais Wade hadi mwaka 2008, amesema alipokea simu ya rais huyo kumpongeza, naye Rais Wade amethibitisha kumpigia simu hiyo Sall.
"Matokeo yanayotoka yanaonesha kuwa Bwana Macky ameshinda. Kama nilivyoahidi siku zote, nilimpigia simu jioni ya leo tarehe 25 Machi kumpongeza." Alisema Wade.
Sall ameiuta ushindi wake kuwa ni ushindi wa watu wa Senegal na kwamba yeye ni rais wa wote. Amesema kwamba dunia inashuhudia kuimarika kwa demokrasia nchini mwake
"Nchi yetu ina demokrasia imara. Tuna raia walio na upeo mkubwa. Wanaojuwa namna ya kufanya maamuzi makini na yanayoonesha dhamana." Amesema Sall.
Shamrashamra katika mji mkuu
Asubuhi ya leo (26.03.2012) ilitandwa kwa shamrashamra na nderemo katika mitaa yote ya mji mkuu, Dakar. Watu walianza kusherehekea hata kabla ya Rais Wade kukubali kushindwa, kwani vyombo vya habari vya serikali vilikuwa vimeshaanza kutoa mfululizo wa matokeo ya uchaguzi uliofanyika hapo jana.
Hofu kwamba Rais Wade, mwenye miaka 85 na ambaye ameitawala nchi Senegal kwa miaka 12, angelijaribu kung'ang'ania madaraka au kuyapinga matokeo ya uchaguzi, ilisababisha mapambano mabaya katika siku za kuelekea kwenye uchaguzi. Wanaharakati wa upinzani walisema hatua ya Wade ya kugombea muhula wa tatu wa urais ilikuwa kinyume na katiba.
Lakini kukubali kushindwa haraka kwa Wade, kunaiongezea nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi sifa zake katika masuala ya kidemokrasia. Wade mwenyewe aliingia madarakani akitokea upinzani kwa kumshinda Rais Abdou Diouf hapo mwaka 2000, ambaye naye alikubali kushindwa baada ya miaka 19 madarakani na akakabidhi madaraka kwa njia za amani.
Ufaransa yaisifu Senegal
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa ndani ya kipindi cha masaa 48 yajayo, lakini tayari salamu za pongezi zimeanza kutolewa kutoka jumuiya ya kimataifa. Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Senegal, imewapongeza watu wa Senegal na kusema kuwa hilo ni jambo zuri kwa nchi hiyo na kwa Afrika nzima.
Akizungumza na kituo cha redio cha Info mapema leo na akilinganisha na yanayotokea sasa nchini Mali, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ameielezea Senegal kama mfano wa demokrasia. "Ukiyatazama yanayotokea Mali, hii ni alama ya kheri kwa Afrika." Amesema Rais Sarkozy.
Katika kampeni zake, Sall aliutumia ugumu wa maisha ya raia walio wengi kama turufu ya kumuangushia Rais Wade, ambaye licha ya kusifiwa kuimarisha miundombinu nchini Senegal, ameshindwa kuinua hali ya maisha ya watu wa kawaida.
Sasa jukumu kubwa la Sall ni kuthibitisha ukweli wa ahadi zake za wakati wa kampeni na pia kuendeleza misingi ya kidemokrasia ya taifa hilo lenye raia milioni 13, na lililowahi kuitwa na kuwa sehemu ya Shirikisho la Mali.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf