Trump asitisha mpango wa wakimbizi Marekani
28 Januari 2017Trump amesema hatua hiyo ni kuwalinda Wamarekani dhidi ya mashambulizi ya kigaidi. Agizo la kuwazuia wageni na kusitisha kutolewa kwa visa kwa wasafiri kutoka Syria, Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan na Yemen litadumu kwa siku tisini zijazo.
Akizungumza katika makao ya wizara ya ulinzi hapo jana, Trump alisema anaanzisha hatua mpya za uchunguzi wa kiusalama ili kuwazuia magaidi wenye itikadi kali za Kiislamu kuingia Marekani na kuongeza wanataka tu watu wanaoipenda nchi yao na kuiunga mkono kuingia nchini humo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na asasi za kiraia zimelaani hatua hizo zilizotajwa kibaguzi na kusema wakimbizi watakwama katika maeneo ambayo si salama na kuichafulia sifa Marekani ambayo imekuwa nchi ya kuwakaribisha wahamiaji. Agizo hilo la rais linapunguza idadi ya wakimbizi watakaopewa hifadhi mwaka huu kutoka 110,000 hadi 50,000.
Hatma ya wakimbizi na wahamiaji mashakani
Athari za agizo hilo zimeanza kusababisha hali ya taharuki miongoni mwa familia za waarabu Wamarekani, wanafunzi, watu walio njiani kuelekea Marekani kwa matibabu na sababu nyingine za kusafiri. Wakati wa kampeini, Trump aliahidi kuchukua hatua kali za kiusalama kuwazuia wanamgambo kuingia Marekani kutokea nchi za kigeni.
Kutanuka kwa kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu IS nchini Syria na Iraq ambalo lilisababisha mmiminiko wa wahamiaji barani Ulaya, pamoja na misururu ya mashambulizi Ufaransa, Ubelgiji na nchi nyingine za Ulaya kutoka kwa wapiganaji wa IS kumeifanya Marekani kusita kuwapokea wakimbizi kutoka Syria ambako kuna vita.
Ikiwa ni siku nane tangu kiongozi huyo mpya wa Marekani kuingia madarakani, tayari ameshatia saini maagizio ya Rais yanayoonekana kuutikisa ulimwengu. Ameagiza maafisa kuanza ujenzi wa ukuta katika mpaka kati ya Marekani na Mexico na kuapa kuwa Mexico ndiyo itagharamia ukuta huo.
Hapo jana alizungumza na Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto kwa njia ya simu, ili kujaribu kutatua tofauti kati yao baada ya kufutiliwa mbali kwa ziara ya kiongozi huyo wiki ijayo nchini Marekani kutokana na suala hilo tete la ujenzi wa ukuta mpakani kuwazuia wahamiaji kuingia Marekani. Taarifa kutoka serikali zote mbili zilisema mazungumzo kati ya viongozi hao yalikuwa ya tija.
Meya wa Berlin amrai Trump kutojenga kuta
Meya wa Jiji la Berlin Michael Mueller ametoa wito kwa Trump asijenge ukuta katika mpaka wa taifa lake na Mexico. Jiji la Berlin liligawanywa kwa ukuta kuanzia 1961 hadi 1989. Ulijengwa na utawala wa kimabavu wa kisoshilisti wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki, lengo likiwa kuwadhibiti wananchi wake kutorokea Magharibi, na kuwa ishara muhimu ya ukandamizaji wakati wa Vita Baridi.
Meya huyo alisema wao kama watu wa Berlin wanatambua sana namna walivyosumbuka na madhara ya mgawanyiko katika eneo hilo ulifanikishwa kwa ukuta wa zege wenye kizuizi cha nyaya za umeme. Alisema kutokana na uzoefu wa kihistoria, wakazi wa Berlin lazima wasikubaliane na wale wote ambao kwa kiasi kikubwa wanataka kuondosha uhuru wao na uhuru wa Wamarekani.
Wakati huo huo, Trump alifanya mkutano wake wa kwanza tangu kuapiswha na kiongozi wa taifa la kigeni, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ambapo viongozi hao wawili wamejadili ushirikiano na umuhimu wa kile walichokitaja mahusiano ya kipekee kati ya mataifa hayo mawili, wajibu wao kwa Jumuiya ya kujihami ya NATO na biashara kati ya nchi hizo mbili, miongoni mwa mambo mengine. Trump ameusifu Uingereza kwa kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya akiutaja uamuzi huo kuwa jambo zuri.
Jumamosi Trump atazungumza kwa njia ya simu na viongozi kadhaa wa dunia akiwemo Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Francois Hollande, Rais wa Urusi Vladimir Putin na Wazuiri mkuu wa Australia Malcolm Turnbull.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp
Mhariri: Sudi Mnette