Tshisekedi ajitangaza rasmi kuwa rais, ataka jeshi limuheshimu
19 Desemba 2011Matangazo
Tshisekedi amewaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa, kwamba serikali ya Rais Joseph Kabila imefutwa kazi na kwamba yeye, Tshisekedi, ndiye atakayeapishwa siku ya Ijumaa. Tshisekedi amewashukuru raia kwa kumchagua na kulitaka jeshi la Kongo kumtii.
Hata hivyo, msemaji wa chama tawala, ameiita kauli hiyo ya Tshisekedi kuwa ni utani mzaha mkubwa na kumuonya dhidi ya kuasi taasisi halali za Jamhuri.
Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu mjini Kinshasa iliamua kuwa Kabila alishinda uchaguzi kwa asilimia 49 ya kura dhidi ya asilimia 32 za Tshisekedi. Waangalizi wa kimataifa wanasema, uchaguzi wa Novemba 28 ulikuwa na dosari kubwa wakitaja matatizo yaliyojitokeza katika kuhisabu kura, na idadi kubwa ya kura ambazo hazikuonekana.