1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika kutuma kikosi maalum cha wanajeshi kukabiliana na mizozo

1 Februari 2014

Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimetangaza (31.01.2014) kutuma kikosi maalumu cha wanajeshi watakaoshughulikia mizozo kwa dharura ili kumaliza umwagaji wa damu katika nchi mbili barani humo zinazokumbwa na mizozo.

https://p.dw.com/p/1B19Q
Picha: Getty Images

Mwenyekiti mpya wa umoja wa Afrika na ambaye ni Rais wa Mauritania Mohammed Ould Abdel Aziz alisema wameamua kuundwa kwa kikosi hicho maalum cha wanajeshi na nchi wanachama ndiyo watakaotoa wanajeshi watakaotekeleza operesheni hizo.

Ahadi hiyo ya kutumwa kwa wanajeshi nchini Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ni kufuatia mkutano wa kilele wa umoja wa Afrika uliokamilika hapo jana mjini Addis Ababa,Ethopia.

Mizozo yatawala mada za mkutano

Mkutano huo ulipaswa kuangazia pakubwa masuala ya kilimo na usalama wa chakula lakini mizozo hiyo ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ndiyo yalitawala mada za mkutano huo uliowaleta pamoja viongozi 34 wa nchi za Afrika.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkozasana Dlamini Zuma
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkozasana Dlamini ZumaPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Rais wa halmashauri ya Umoja huo Nkosazana Dlamini Zuma amethibitisha kuwa nchi tisa tayari zimeahidi kutuma wanajeshi wao katika nchi hizo.Nchi zilizojitolea kutoa wanajeshi katika kikosi hicho maalum ni Algeria ,Angola, Chad, Ethiopia, Guienea, Mauritania, Afrika Kusini, Tanzania na Uganda.

Hata hivyo Zuma hakufafanua ni lini hasa kikosi hicho kitaanza kazi au kitakuwa na idadi ya wanajeshi wangapi.Viongozi hao pia wameamua kuwa waangalizi wanapaswa kwenda nchini Sudan Kusini kuhakikisha kuwa mkataba wa kusitisha mapigano unatekelezwa.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko miezi 10 baada ya waasi kuipindua serikali na kuchoceha mapigano kati ya makundi ya waasi wa kiislamu na wakristo.

Mauaji yaendelea kuripotiwa CAR

Licha ya kuwepo kwa serikali mpya inayoongozwa na Rais Catherine Samba Panza,machafuko yameendelea kuripotiwa katika mji mkuu Bangui.Shirika la msalaba mwekundu nchini humo hapo jana lilisema kiasi ya watu 30 wameuaw katika machafuko katika kipindi cha siku tatu zilizopita.

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba PanzaPicha: Reuters

Sudan Kusini ilijikuta katika mapigano baada ya kuibuka tofauti kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar aliyemfuta kazi mwaka jana.Mapigano yanaendelea kuripotiwa hasa katika majimbo yenye utajiri wa mafuta licha ya makubaliano ya kustisha vita.

Hii leo Jumamosi kunatarajiwa kufanyika mkutano wa wafadhili watakaochangisha fedha za kukisaidia kikosi cha wanajeshi 5,000 wa umoja wa Afrika kilichoko Jamhuri ya Afrika ya Kati MISCA.

Umoja wa Ulaya ambao uliidhinisha wiki hii kupelekwa kwa kikosi cha wanajeshi 500 Jamhuri ya Afrika ya Kati umeahidi msaada wa euro milioni 61 hapo jana kusaidia shughuli za kijeshi na mchakato wa kisiasa nchini humo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo