Urusi: Jenerali wa ulinzi wa nyuklia Igor Kirillov auawa
17 Desemba 2024Wachunguzi wamethibitisha kifo cha jenerali huyo aliyekuwa kiungo muhimu katika vita vya Urusi nchini Ukraine, huku Ukraine ikisema mauaji hayo ni matokeo ya operesheni maalum ya Kiev ndani ya ardhi ya Urusi.
Kirillov, mwenye umri wa miaka 54, alikuwa mkuu wa kitengo kinachotoa ulinzi dhidi ya vitisho vya nyuklia, silaha za kemikali na za kibaolojia.
Msemaji wa Kamati ya Uchunguzi ya Shirikisho la Urusi, Svetlana Petrenko, amesema mripuko huo ulisababishwa na bomu lililotegwa kwenye baiskeli ya umeme karibu na jengo la makaazi ya watu, kusini mashariki mwa mji mkuu, Moscow.
Unaweza kusoma pia: Uingereza yaiadhibu Urusi kwa kutumia silaha za kemikali nchini Ukraine
Likimnukuu afisa wa usalama, shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi, TASS, limeripoti kwamba bomu hilo lilikuwa na uzito gramu 300 za kemikali, sawa na bomu aina ya TNT.
Hata hivyo, undani wa shambulio hilo haujaubainika na kulingana na Petrenko, wachunguzi wamefika katika eneo la mkasa kufanya uchunguzi wao.
"Idara Kuu ya Upelelezi ya Kamati ya Uchunguzi ya Urusi ya Moscow inachunguza kesi ya jinai kuhusu kifo cha wanajeshi wawili. Kikosi cha uchunguzi kinafanya kazi katika eneo la tukio, kubaini mazingira ya uhalifu na watu waliohusika. Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi ya Urusi alifahamishwa juu ya hatua za awali za uchunguzi na hali ilivyo. Mkuu wa idara alitoa maagizo kadhaa na kuamuru uchunguzi uwe chini ya udhibiti wa ofisi kuu ya Kamati ya Uchunguzi," amesema Petrenko.
Unaweza pia kusoma: Trump aahidi tena kumaliza "mauaji" ya vita vya Ukraine
Kulingana na picha za eneo la mkasa, mlango wa jengo palipotokea mripuko huo uliharibika sana.
Chanzo cha habari chasema Ukraine imehusika na kifo cha Kirillov
Chanzo kimoja kutoka Shirika la Ujasusi la Ukraine, SBU, kimelithibitishia shirika la habari la Reuters kwamba SBU imehusika na shambulio hilo. Chanzo hicho kimesema baiskeli ya umeme iliyotegwa bomu hilo iliripuliwa na kumuua Kirillov na msaidizi wake, wakati wakitoka kwenye jengo la mtaa wa Ryazansky Prospekt mjini Moscow.
Unaweza kusoma pia: Mawaziri wa EU wasaini vikwazo vipya dhidi ya Russia
Kirillov aliyetizamwa kama miongoni mwa wahamasishaji wakuu wa vita vya Urusi, alidai kuwa Ukraine ilikuwa ikitengeneza kile alichokiita kuwa "bomu chafu".
Mabomu machafu ni silaha za maangamizi makubwa zinazojumuisha viripuzi vya kawaida na vyenye mionzi. Hakujakuwa na uthibitisho wowote wa Ukraine kuwa au kuunda silaha kama hizo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin pia aliwahi kutoa madai kama hayo dhidi ya Ukraine akijikita kwenye ripoti zilizotolewa na Kirillov ambaye yuko kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo na nchi za Magharibi.
Mnamo Desemba 16, idara ya usalama ya Ukraine, ilimshutumu Kirillov kwa kutumia silaha za sumu zilizopigwa marufuku, wakati wa operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine iliyoanza Februari 2022.
Mnamo mwezi Mei, Marekani pia iliishutumu Urusi kwa kutumia sumu aina ya chloropicrin dhidi ya wanajeshi wa Ukraine kinyume na Mkataba wa Silaha za Kemikali (CWC).
(DPAE, APAE)