1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Assad waporomoka - Hijab

14 Agosti 2012

Aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria na ambaye sasa amekimbia nje ya nchi hiyo, amesema utawala wa Assad unaporomoka, licha ya kujijengea picha kwamba bado ni imara.

https://p.dw.com/p/15pRU
Waziri Mkuu wa zamani wa Syria, Riyad Hijab.
Waziri Mkuu wa zamani wa Syria, Riyad Hijab.Picha: Reuters

Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari, Riyad Hijab amesema kwamba, baada ya miezi 17 ya maandamano dhidi ya serikali, utawala wa Assad umedhoofika sana. Katika mkutano huo uliofanyika mjini Amman, Jordan, Hijab amesema kwa uzoefu wake, utawala huo unaporomoka kimaadili, kivifaa na kiuchumi.

Ingawa ni vigumu kuthibitisha idadi ya maeneo ambayo waasi wanayadhibiti, lakini ushahidi wa kimazingira unaonesha kuwa Assad amepoteza baadhi ya maeneo ya mpakani, kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo, na mapigano yamedhoofisha sana nguvu zake katika miji mikubwa kama vile Aleppo na Homs.

Hijab amewasifu waasi kwamba mapinduzi yao yamekuwa "kigezo cha juhudi na kujitoa muhanga kwa ajili ya uhuru na heshima." Ingawa Hijab hakuwa sehemu ya watu muhimu wanaomzunguka Assad, lakini akiwa waziri mkuu na afisa wa ngazi za juu, kuondoka kwake kumekuwa pigo kubwa kwa utawala huo na kuongeza morali kwa upande wa waasi.

Hata hivyo, kwenye medani ya kivita ukweli bado haujabadilika. Bado wanajeshi wa serikali wanashambulia kwa kutumia ndege na mizinga. Hijab aliwataka maafisa wa jeshi kujiunga na upinzani na pia makundi mbali mbali ya waasi kuungana dhidi ya utawala wa Assad ambao ameuita "adui wa Mungu."

Uturuki yaendelea na mazoezi ya kijeshi mpakani

Hayo yanatokea katika wakati ambao Uturuki imefanya mazoezi mapya ya kijeshi karibu na mpaka wake na Syria, kwa mujibu wa shirika la habari la Uturuki, Anatolia. Leo vifaru vya Uturuki vimefanya mazoezi ya kutunga shabaha za mbali katika mpaka wa Oncupinar, kusini ya jimbo la Kilis.

Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki.
Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki.Picha: Reuters

Mazoezi hayo yanafuatia mengine ambayo yamekuwa yakifanyika kwa siku kadhaa sasa, baada ya serikali Uturuki kusema ingeliwafuata waasi wa Kikurdi hadi ndani ya ardhi ya Syria.

Hata hivyo, vyombo vya habari nchini Uturuki vimeyatafsiri mazoezi hayo kama maonyesho ya nguvu za Uturuki mbele ya Syria, ambayo inaituhumu kuwasaidia Wakurdi wa Syria kuishambulia Uturuki.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili uliingia mashakani zaidi mwishoni mwa mwezi Juni, baada ya Syria kuiangusha ndege ya kijeshi ya Uturuki na kuwaua marubani wake wawili. Tangu wakati huo, Uturuki imeiita Syria kuwa hasimu wake, huku Syria ikisema Uturuki inawahifadhi na kuwafadhili wanajeshi wanaoasi na kukimbia jeshi la Syria.

Waliokufa sasa wapindukia 23,000

Zaidi ya wakimbizi 60,000 wa Syria wako nchini Uturuki kukimbia machafuko nyumbani kwao. Hadi jana, zaidi ya watu 23,000 walishauawa nchini Syria tangu kuanza kwa maandamano dhidi ya serikali Machi mwaka jana.

Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria, chombo cha kijeshi cha upinzani.
Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria, chombo cha kijeshi cha upinzani.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Haki za Binaadamu la Syria iliyotolewa leo, 16,142 kati yao ni raia, 1,018 wanajeshi walioasi na 5,842 wanajeshi wa serikali.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdel Rahman, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hesabu hiyo haijumuishi maelfu ya mahabusu ambao hatima yao haijuilikani wala wanamgambo wa shabiha, wanaoiunga mkono serikali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/PDA/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman