Vikosi vya Israel vyakaribia mji mkuu wa Syria, Damascus
10 Desemba 2024Israel ilikamata eneo la ulinzi kusini mwa Syria na kuanzisha mashambulizi ya anga kwenye ngome za jeshi la Syria. Operesheni ya jeshi la Israel ndani ya Syria inajiri siku chache tu baada ya Rais Bashar al-Assad kuangushwa na muungano wa waasi.
Chanzo cha usalama cha Syria kimesema askari wa Israel wamefika mji wa Qatana, ambao uko kilomita 10 ndani ya mipaka ya Syria mashariki mwa eneo lisilo na ulinzi wa kijeshi linalotenganisha Milima ya Golan linalokaliwa na Israel, na Syria.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Israel amekanusha taarifa hizo. Israel imesema haitahusika na mgogoro nchini Syria na kwamba kukamata kwake eneo hilo la ulinzi ni hatua ya kujilinda.
Misri, Qatar na Saudi Arabia zimelaani uvamizi huo. Vyanzo vya kikanda vya usalama na maafisa ndani ya jeshi lililoangushwa la Syria wamesema mashambulizi ya anga ya Israel yaliendelea kote Syria usiku kucha yakivilenga vituo vya kijeshi.
Mashambulizi hayo yameharibu helikopta na ndege za kivita pamoja na mali za jeshi la Syria ndani na karibu na mji mkuu, Damascus.