1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa OSCE wakutana kwa mazungumzo Malta

5 Desemba 2024

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE wanakutana nchini Malta kujadiliana mambo mbalimbali ya kiusalama huku wakilaumiana kuhusu vita vya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4nns0
Malta | Mkutano wa viongozi wa OSCE
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE wanaokutana nchini Malta: 05.12.2024Picha: Alberto Pizzoli/AP Photo/picture alliance

Viongozi hao wa OSCE wametupiana lawama hasa kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amemtuhumu mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kwa kueneza habari potofu huku akiilaumu Moscow kuzidisha makali katika vita vya Ukraine, hasa kutokana na kutumwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini na mashambulizi makubwa yaliyolenga miundombinu ya nishati ya  Ukraine.

Viongozi hao wawili ambao hawatarajii kufanya mazungumzo ya pande mbili, walikuwa Malta kushiriki mkutano wa kila mwaka wa mawaziri wa Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Lavrov katika nchi ya Umoja wa Ulaya tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.

Lawama kama hizo zimetolewa pia na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ambaye amesema kuwa Moscow inajihusisha na mchezo mbaya wa kuhatarisha usalama wa Ulaya, huku yule wa Poland Radoslaw Sikorski akitaka uanachama wa Urusi katika jumuiya hiyo usitishwe kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Majibu ya Urusi na kauli ya mwenyeji Malta

Malta | Lavrov akihudhuria mkutano wa OSCE
Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov (akiangalia juu) wakati wa Mkutano wa OSCEPicha: Alberto Pizzoli/AP Photo/picture alliance

Urusi kwa upande wake imeituhumu Marekani kwamba ina nia ya kuvuruga utulivu katika kanda ya Asia mashariki huku ikizilaumu nchi za Magharibi kwa kupuuza miito ya Rais Vladimir Putin ya kutopeleka wanajeshi zaidi nchini Ukraine. Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameendelea kuwa nchi za Magharibi zimeanzisha zama mpya za Vita Baridi na kuonya kwamba hilo linaweza kugeuka na kuwa vita halisi kati ya Mashariki na Magharibi.

Soma pia: Urusi yaonyesha kutojali mustakabali wa OSCE

Kwa upande wake Ian Borg Waziri wa Mambo ya Nje wa Malta na Mwenyekiti wa OSCE amewataka viongozi kuheshimu kanuni za jumuiya hiyo kwa kusema mataifa yote wanachama yana haki ya kushiriki kikamilifu kwenye mkutano huo.

"Sio suala la Malta kuwa na sababu yoyote ya kumualika Lavrov. Jumuiya ya OSCE ina nchi wanachama 57, na nchi zote 57 zilikubaliana kwamba mkutano huu ufanyike na kuhudhuriwa na wanachama wote 57. Malta imetekeleza kilichoombwa na wengi, na wengi wameishukuru Malta kwa kuandaa mkutano huu wa mawaziri. Na hivyo ndivyo Urusi ilivyoalikwa. Mwezi Septemba, Waziri Lavrov alihudhuria huko New York, Marekani mkutano wa Umoja wa Mataifa, na hivyo ndivyo yanavyofanya kazi mashirika," alisisizita Borg.

Soma pia: Lavrov ziarani Malta

OSCE ni jumuiya ya kikanda ya usalama ambayo ni kubwa zaidi duniani na hutumiwa kufanya maamuzi makubwa. Mawaziri hao wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo wanaokutana Malta watatumia jukwaa hilo muhimu kujadili na kushughulikia masuala ya usalama katika eneo la Ulaya na Asia-Mashariki.

Malta inashikilia kwa mara ya kwanza uenyekiti wa kupokezana wa Jumuiya hiyo ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya. Katika ulimwengu unaoshuhudia mabadiliko kwenye siasa za kijiografia, vitisho na changamano za kiusalama, na wasiwasi wa kimataifa, OSCE ina jukumu muhimu katika kuyapa kipaumbele mazungumzo, kuimarisha usalama, ustawi na ushirikiano kati ya nchi wanachama.

(Vyanzo: AP,DPAE, Reuters, AFP)