1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa waasi wa DRC wapanda kizimbani ICC

24 Novemba 2009

Viongozi wa makundi ya waasi wa Kongo Germain Katanga na Matheiu Ngudjolo Chui wanafikishwa mahakamani hii leo katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya ICC iliyoko The Hague,Uholanzi.

https://p.dw.com/p/Ke8M
Majaji wa mahakama ya ICC,The HaguePicha: AP

Waasi hao wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita na wa kibinadamu baada ya kulisimamia shambulio la mwaka 2003 dhidi ya kijiji kimoja katika eneo la Ituri lililoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Hii ni kesi ya pili inayosikilizwa katika Mahakama hiyo ya kudumu ya kimataifa.Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita na kibinadamu baada ya kuwashambulia raia wa kawaida,kuwabaka wanawake vilevile kuwasajili na kuwatumia watoto vitani katika kijiji cha Bogoro kilichoko Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo.

Shambulio hilo lilitokea wakati wa mapambano kati ya makundi hasimu ya waasi yaliyokuwa yakingangania usimamizi wa migodi ya dhahabu na almasi na maeneo ya mafuta.

Niederlande Menschenrechte Germain Katanga vor dem Strafgerichtshof in Den Haag
Kamanda wa zamani wa kundi la Patriotic Resistance Force, Germain KatangaPicha: AP

Germain Katanga aliye na umri wa miaka 31 na wa kabila la Ngiti anadaiwa kuwa aliwasimamia wapiganaji wa kundi la waasi la Patriotic Resistance Force naye Matheu Ngudjolo Chui aliye na umri wa miaka 39 wa kabila la Lendu anadaiwa kuwa kiongozi wa kundi la waasi la National Integrationist Front,FNI.Watuhumiwa hao wameyakanusha mashtaka yote yanayowakabili,saba ya uhalifu wa kivita na matano dhidi ya ubinadamu . Kiasi cha watu alfu 8 waliuawa katiia shambulio hilo. Waasi hao wawili waliwasajili na kuwatumia watoto vitani waliokuwa na umri wa chini ya miaka 15.Profesa Christoph Safferling wa Chuo Kikuu cha Marburg cha Ujerumani aliye pia Mkurugenzi wa Taasisi inayohusika na utafiti na uhifadhi wa masuala ya kesi za uhalifu wa kivita anaielezea hatua hii''Ukiizingatia misingi ya kusawazisha mambo hatua hii imepokelewa vizuri.Hata hivyo kuna matatizo yatakayojitokeza pengine kwasababu kesi hii si rahisi hasa ukizingatia kuwa waathirika wengi watapata nafasi ya kutoa ushahidi katika mahakama ya kimataifa ya ICC.Ni shughuli ambayo itachukua muda mrefu.''

Mwendesha mashtaka katika mahakama hiyo ya ICC tayari ameshafutilia mbali mashtaka ya utumwa unaoegemea ngono na kudhalilishwa kabla hata ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.Ni suala linalovunja moyo ila huenda lilikubaliwa baada ya kusikilizwa kwa kesi iliyomkabili Radovan Karadzic aliyehusika katika mauaji ya raia wengi wa Serbia iliyosikilizwa katika Mahakama ya ICTY. Katika kesi hii inayomkabili Kanali Katanga mazingira yanafana ila kwa kiasi kidogo na mahakama itajitahidi kulithibitisha shtaka hilo.Profesa Safferling anafafanua kuwa,''Mshtakiwa sasa ameshafikishwa katika mahaka ya kimataifa ya ICC,mazingira ya Katanga na Chui yanafanana na yale ya kesi ya Karadzic ila kwa kiasi kidogo.Kwahiyo huenda ikajikita zaiidi katika masuala mengine.''ameeleza.

Kongo Milizenführer Thomas Lubanga in Den Haag vor Gericht
Mshukiwa wa kwanza ya ICC Thomas LubangaPicha: AP

Mahakama ya ICC kwa sasa inazichunguza kesi nyengine nne za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja na uhalifu uliotokea katika eneo la Darfur la Sudan,Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati.Mahakama ya ICC ilisikiliza kesi yake ya kwanza mwaka 2008.Kiongozi wa waasi wa Kongo Thomas Lubanga ametuhumiwa kwa kuwatumia watoto katika vita katika kundi lake la Union of Congolese Patriots lililokuwa likiendesha shughuli zake katika eneo la Mashariki ya Kongo la Ituri.Hati ya kumkamata Bosco Ntaganda aliyekuwa pia katika kundi hilo ilitolewa mwezi Agosti mwaka 2006.Hata hivyo mpaka sasa bado anasakwa na Mahakam hiyo ya kimataifa.Kesi hiyo inanatarajiwa kusikilizwa kwa muda wa miaezi kadhaa.

Mwandishi:Jürgen Kleikamp/ZR/ Thelma Mwadzaya

Mhariri:Othman Miraji