1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Waasi wa Syria waingia Damascus, wasema Assad amekimbia

8 Desemba 2024

Waasi nchini Syria wamedai kuwa rais wa Syria Bashar al-Assad amekimbia nchi hiyo baada ya waasi hao kuchukua udhibiti wa mji mkuu Damascus.

https://p.dw.com/p/4nsyq
Bürgerkrieg in Syrien
Picha: Omar Ibrahim/REUTERS

Waasi nchini Syria wamedai kuwa rais wa Syria Bashar al-Assad amekimbia nchi hiyo baada ya waasi hao kuchukua udhibiti wa mji mkuu Damascus.

Baada ya kuuteka mji wa Damascus, waasi wa Syria wametangaza kupindua serikali ya Rais Bashar al-Assad na utawala wa chuma wa kiongozi huyo ambaye amekuwa madarakani kipindi ambacho taifa hilo la Mashariki ya Kati limekuwa likizongwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka 10.

Hatua ya waasi hao pia ni pigo kubwa kwa ushawishi wa Urusi na Iran ambao wamekuwa washirika wa karibu wa Assad katika kanda hiyo.

Mapema Jumapili, kamandi ya jeshi la Syria iliwaarifu maafisa wake kwamba utawala wa Assad umekwisha. Hayo ni kulingana na afisa mmoja aliyepokea habari hiyo na baadaye kuliambia shirika la Habari la Reuters.

Lakini baadaye, jeshi la Syria lilisema linaendelea na operesheni dhidi ya "makundi ya kigaidi” katika miji muhimu ya Hama, Homs na Deraa.

Waasi Syria watangaza kuwaachilia huru wafungwa

Maafisa wawili wa ngazi ya juu katika jeshi la Syria wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Assad alikimbia nje ya Damascus bila kujulikana amekwenda wapi, huku waasi wakitangaza kwamba wamechukua udhibiti wa Damascus na hakuna dalili ya uwepo wa vikosi vya jeshi katika mji huo.

Soma pia: Waasi Syria waitwaa Daraa

"Tunasherehekea pamoja na raia wa Syria, habari ya kuachiliwa huru kwa wafungwa wetu, na kutangaza mwisho wa enzi ya dhuluma katika gereza la Sednaya,” waasi wamesema, wakirejelea gereza kubwa nje ya viunga vya Damascus ambako serikali ya Syria imekuwa ikiwafunga maelfu. Utawala wa Assad umehusishwa pakubwa na ukandamizaji dhidi ya upinzani na demokrasia.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria
Mashahidi wamesema maelfu ya watu walijitokeza mjini Damascus wakipaza sauti zao wakisema "uhuru” kutoka nuru karne ya utawlaa wa familia ya Assad.Picha: Omar Sanadiki/AP/dpa/picture alliance

Muungano wa waasi wa Syria umesema unaendelea na kazi ya kukabidhi Madaraka kwa utawala wa mpito na kuupa mamlaka kamili.

"Mapinduzi makubwa ya Syria yanatoka katika hatua ya mapambano ya kuupindua utawala wa Assad na kuelekea katika juhudi za kuijenga Syria ambayo imeungana pamoja ili kufaidi raia wake,” taarifa hiyo iliongeza.

Soma pia: Waasi wa Syria waendelea kusonga mbele

Umoja wa Mataifa wasema Syria ipo katika 'hali tete'

Mnamo Jumapili, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Geir Pedersen amesema "Syria ipo katika wakati mgumu sana” baada ya waasi kukamata Damascus na kumaliza utawala wa miongo mitano ya utawala wa Baath.

Akizungumzia takriban miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, Pedersen amesema kwenye taarifa kwamba "leo tunatazamia kwa matumaini makubwa, mwanzo mpya wa amani, upatanisho, utu na ushirikishwaji kwa Wasyria wote."

Kulingana na mkuu wa shirika la upinzani la uangalizi wa vita Syria, linaloangazia pia masuala ya haki za binaadamu, Rami Abdurrahman, rais Assad aliabiri ndege Jumapili asubuhi kutoka Damascus na kuondoka nchini.

Soma pia: Hamas yathibitisha kuanza kwa mazungumzo ya kusitisha vita Gaza

Hata hivyo hadi sasa serikali ya Syria, haijatoa taarifa yoyote rasmi juu ya kuondoka kwake.

Hii ni mara ya kwanza wapiganaji wa upinzani kuingia Damascus tangu mwaka 2018 wakati vikosi vya Syria vilipoyatwaa tena maeneo yaliyo nje ya mji huo kufuatia mzingiro wa mwaka mmoja.

Siku moja kabla ya kuingia Damascus, wapiganaji hao waliudhibiti mji wa Homs, mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo huku vikosi vya serikali vikiuhama mji huo.

(Reuters,AFPE)