Wafungwa 600 waachiwa huru katika gereza la Makala Kongo
22 Desemba 2024Mamlaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema imewaachilia huru wafungwa 600 katika gereza kuu la nchi hiyo la Makala siku ya Jumamosi kama sehemu ya mchakato unaolenga kupunguza msongamano katika magereza nchini humo.
Waziri wa sheria, Constant Mutamba ametangaza hatua hiyo wakati wa sherehe katika Gereza hilo la Makala katika mji mkuu wa Kongo, Kinshasha huku akiongeza kwamba serikali ya nchi hiyo ipo katika mipango ya ujenzi wa gereza jipya huko Kinshasa.
Soma zaidi. Rais wa Kongo afanya mabadiliko makubwa jeshini
Katika ripoti ya hivi karibuni ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ni kwamba gereza la Makala ambalo ndio gereza kubwa zaidi nchini Kongo linao uwezo wa kuchukua watu 1,500 lakini linawashikilia zaidi ya wafungwa 12,000, wengi wao wakiwa bado wanasubiri kesi zao kusikilizwa.
Mapema mwezi huu wafungwa katika gereza hilo walifanya jaribio la kutoroka katika gereza hilo na watu 129 walikufa. Wapo waliopigwa risasi na walinzi na askari na wengine walikufa kutokana na mkanyagano katika kituo hicho kilichojaa watu.