Wanaharakati wa Syria wataandamana pia Ramadhan
29 Julai 2011Mapigano yameripuka jana usiku kati ya watumishi wa kijeshi wa idara ya upelelezi na wakaazi wa mji wa Dair az Zour, mashariki ya Syria, baada ya waandamanaji watano kuuliwa hapo awali katika eneo hilo kunakokutikana visima vya mafuta na gesi vya Syria.
Dair az Zour, mji wenye wakaazi wasiozidi laki moja na 30 elfu, ulioko katika bonde la Mto Euphratis, mnamo wiki za hivi karibuni uligeuka kitovu cha maandamano dhidi ya utawala wa rais Bashar al Assad.
Shirika rasmi la habari la Syria-Sana, limeripoti, kwa upande wake, bila ya kutoa ufafanuzi kwamba "waharibifu" wamelenga bomba la mafuta karibu na Homs, mji wa wakaazi zaidi ya milioni moja, ulioko kati kati ya nchi hiyo.
Gavana wa Homs, Ghassan al Adel, amesema raia kadhaa wa eneo hilo waliusikia mripuko huo uliotokea leo asubuhi.
Kimoja kati ya vinu viwili vya kusafishia mafuta nchini Syria kinakutikana Homs, kitovu cha maandamano dhidi ya utawala wa rais Bashar al Assad uliotuma vifaru kuuvunja nguvu uasi huo.
Shambulio dhidi ya bomba hilo la mafuta ni la pili la aina yake nchini Syria baada ya lile la July 13 iliyopita katika mji wa Mayadin.
Shambulio dhidi ya pomba la mafuta karibu na Homs limesadif muda mfupi tuu kabla ya wanaharakati kutoa mwito wa kuendelea na maandamano baada ya sala ya ijumaa hii leo.
Wanaharakati wa Syria wametoa mwito pia wa kuendelea na maandamano yao hata katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza jumatatu ijayo.
Katika taarifa yao kupitia Facebook,wanaharakati wapenda mageuzi nchini Syria wamesema maandamano yao yatafanyika kila siku katika mwezi wa Ramadhan kuanzia usiku hadi juwa linapochomoza.
Shirika la haki za binaadam nchini Syria linasema wanajeshi wameingia katika mitaa kadhaa ya mji mkuu wa Damascus na hasa Jouber, na kuwakamata wanaharakati15 wamekamatwa mbele ya msikiti, kunakoanzia maandamano ya kila siku ya ijumaa.
Njia za mawasiliano ya simu na mtandao wa internet zimekatwa tangu alfajiri katika mtaa wa Qadam, kusini mwa Damascus na risasi zimekuwa zikisikika pia tangu vikosi vya usalama vilipoingia katika eneo hilo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp,/Reuters/dpa
Mhariri: Miraji Othman