Wasiwasi umetanda Venezuela kabla Maduro kuapishwa
8 Januari 2025Siku moja kabla ya kuapishwa kwa Rais Nicolas Maduro kwa muhula wa tatu licha ya matokeo ya uchaguzi kukataliwa na upinzani na jumuiya ya kimataifa.
Kiongozi wa upinzani aliye uhamishoni Edmundo Gonzalez Urrutia ameapa kurejea nyumbani kudai kiti cha urais anachosisitiza kuwa alishinda katika uchaguzi wa Julai mwaka jana, huku wafuasi wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi kwa maandamano kabla ya hafla za Ijumaa.
Soma pia: Kiongozi wa upinzani aapa kuzuia mipango ya Maduro ya kuapishwa madarakani
Wakati huo huo wanaounga mkono vuguvugu tawala la Maduro la "Chavista" wameapa kuingia mitaani pia, na tayari maelfu ya polisi na wanajeshi wenye silaha nzito wametumwa katika mji wa Caracas.
Waziri wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello amesema waandamanaji wanaompinga Maduro, ambao aliwataja kuwa "mafashisti" na "magaidi," "watajuta" kujitokeza, na kuapa kwamba wataendelea na mashambulizi ya kukabiliana.
Ukatili dhidi ya waandamanaji
Ukandamizaji wa kikatili dhidi ya waandamanaji baada ya kutangazwa ushindi wa Maduro miezi mitano iliyopita ulisababisha watu 28 kuuwawa, wengine 200 kujeruhiwa na zaidi ya 2,400 kukamatwa.
Rais Maduro siku ya Jumanne alitangaza kukamatwa kwa wageni saba -- wakiwemo Wamarekani wawili -- ambao aliwashutumu kuwa "mamluki" wanaojaribu kumzuia kuapishwa kwa miaka mingine sita madarakani.
Soma pia: Venezuela yawashikilia raia saba wa kigeni kwa madai ya njama ya kumuua Rais Maduro
Aidha rais huyo ameamuru kusambazwa kwa vikosi vya uslama nchini kote kabla ya kuapishwa:
"Nguvu zote za kisiasa za Venezuela, nguvu zote maarufu, Jeshi zima la Kitaifa la Bolivia, Wanamgambo wote wa Kitaifa wa Bolivia kama sehemu maalum, na vikosi vyote vya polisi vitaamilishwa kuanzia leo usiku, mnamo tarehe 8 na 9, katika nchi nzima. "
Urrutia atafuta uungwaji mkono
Wakati joto la likisiasa likiendelea kufukuta Venezuela, kiongozi wa upinzani Gonzalez Urrutia alikuwa akimalizia ziara ya kimataifa ambayo imempeleka Argentina, Uruguay na Marekani -- ambako alipata uungwaji mkono kutoka kwa Rais Joe Biden siku ya Jumatatu.
Soma pia:Nchi za G7 zamuunga mkono kiongozi wa upinzani wa Venezuela
Atatembelea pia Panama, ambapo atakutana na marais wa zamani wa Amerika ya Kusini na mawaziri kadhaa wa sasa wa mambo ya nje Jumatano kama sehemu ya kampeni ya kushinikiza Maduro kujiuzulu.
Lakini iwapo atatua Venezuela mamlaka ya Caracas imeapa kumkamata, baada ya kuwa uhamisho nchini Uhispania tangu mwezi Septemba mwaka jana.
Kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado, ambaye Gonzalez Urrutia alimbadilisha kama mgombea urais dakika za mwisho baada ya kuzuiwa na mamlaka kugombea, amesema atatoka mafichoni kuungana na waandamanaji Alhamisi.