Watu 28 wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
22 Desemba 2024Shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza limesema mashambulizi ya Israel ya usiku na mapema leo Jumapili yamewaua Wapalestina wasiopungua 28, mashambulio hayo yamelenga nyumba ya familia moja na jengo la shule lililokuwa likitumika kuwahifadhi watu waliokimbia vita na ambalo jeshi la Israel limesema lilitumiwa na kundi la Hamas.
Msemaji wa shirika la hilo la kiraia Mahmud Bassal amesema katika taarifa kwamba watu wasiopungua 13 wameuawa kwa shambulio la anga la Israel kwenye nyumba ya familia ya bwana aliyefahamika kama Abu Samra katikati mwa eneo la Gaza la Deir el-Balah. Bassal ameongeza kuwa mashambulizi hayo pia yamewaua watu nane wakiwemo watoto wanne katika jengo la shule.
Soma zaidi. Netanyahu atoa oanyo kali kwa Wahouthi wa Yemen
Jeshi la Israel kwa upande wao limesema limefanya mashambulizi hayo ya usiku kucha likiwalenga wanamgambo wa Hamas wanaoendesha shughuli zao huko. Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas ni kwamba takriban watu 45,227 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa vita hivyo.