1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu atoa oanyo kali kwa Wahouthi wa Yemen

19 Desemba 2024

"Wahouthi wanajifunza, na watajifunza kwa njia ngumu kwamba yeyote anayeishambulia Israel hulipa gharama kubwa sana," asema Netanyahu

https://p.dw.com/p/4oNI4
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa israel
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa israelPicha: Uncredited/Israeli Government Press Office/AP/dpa/picture alliance

Shambulizi la angani la Israel mapema Alhamisi Ukanda wa Gaza limewaua watu watano, wakiwemo wavulana wawili na wanawake wawili, na kujeruhi saba.

Israel pia imefanya operesheni nchini Yemen, ikishambulia bandari na miundombinu ya nishati, ambapo watu tisa wameuawa. Wakati huo huo, Shirika la Human Rights Watch limeishutumu Israel kwa "mauaji ya halaiki ya Wapalestina." Rais Vladimir Putin pia ametaka Israel iondoe vikosi vyake kutoka Syria. 

Watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulizi la Israel kwenye kambi ya wahamiaji ya Maghazi, Ukanda wa Gaza, walipelekwa katika hospitali ya Aqsa, ambapo maafisa walithibitisha vifo vyao. Mwandishi wa shirika la Associated Press alihesabu miili mitano ya waliouawa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Wapalestina inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya vifo kutokana na vita Ukanda wa Gaza imezidi 45,000. Wizara hiyo haijatofautisha kati ya vifo vya wanamgambo na raia lakini imesema nusu ya waliouawa ni wanawake na watoto. 

Shambulizi linalodaiwa kupiga eneo la kambi ya wahamiaji Maghazi Ukanda wa gaza limesababisha vifo vya watu watano. (Picha ya maktaba)
Shambulizi linalodaiwa kupiga eneo la kambi ya wahamiaji Maghazi Ukanda wa gaza limesababisha vifo vya watu watano. (Picha ya maktaba)Picha: Omar Ashtawy/APA Images/Zumapress/picture alliance

Israel yafanya operesheni ya kijeshi Yemen

Mapema Alhamisi, Israel pia ilishambulia ngome za waasi wa Kihouthi nchini Yemen, na kusababisha vifo vya watu tisa, kulingana na maafisa wa Israel. Jeshi la Israel limesema operesheni hiyo, iliyopangwa awali, ilihusisha ndege za kivita 14. 

Mashambulizi hayo yalitokea wakati kombora lililofyatuliwa na waasi wa Kihouthi kutoka Yemen lilidunguliwa, lakini vipande vyake vilianguka na kuharibu vibaya shule moja karibu na mji wa Tel Aviv. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ametoa onyo kali kwa waasi wa Kihouthi kufuatia shambulizi hilo. 

" Baada ya Hamas, Hezbollah, na utawala wa Assad wa Syria, Wahouthi kundi la mwisho liliosalia katika mhimili wa uovu wa Iran. Wanajifunza, na watajifunza kwa njia ngumu kwamba yeyote anayeishambulia Israel hulipa gharama kubwa sana," amesema Netanyahu.

Israel ilitangaza vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas walioishambulia mnamo Oktoba 7, 2023 na kuua watu 1,200 na kuwashika mateka 250.

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

HRW yaituhumu Israel kwa "mauaji ya kimbari" ya Wapalestina

Katika tukio jingine, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeishutumu Israel kwa kusababisha vifo vya maelfu ya Wapalestina kwa kuhujumu mifumo ya maji, kitendo ambacho shirika hilo kimetaja kuwa ya "mauaji ya halaiki."

Tuhuma hiyo ni ya hivi karibuni zaidi miongoni mwa shutuma kama hizo dhidi ya Israel kuhusiana na vita vyake Gaza.

Israel hukanusha vikali shutuma hizo ikisema vita vyake vinawalenga wanamgambo wa Hamas wala si raia wa Gaza.

Kwingineko rais wa Urusi Vladimir Putin amesema ni matumaini yao kwamba Israel itaondoka Syria, lakini kwa sasa inapeleka vikosi zaidi huko.

Kuhusu uwepo wa vikosi vya Urusi nchini Syria, amekariri nia ya nchi yake kuendelea kuwa na kambi za kijeshi Syria baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.

Kwenye mkutano wake wa kila mwisho wa mwaka na waandishi habari, Putin amesema mazungumzo ni sharti yafanywe na vikosi vya waasi ambavyo ndivyo kwa sasa vinadhibiti Syria.

Hata hivyo hakugusia ripoti kuhusu madai kwamba inahamisha vikosi vyake kutoka Syria kuvipeleka Libya.

(APAE, DPAE, EBU)