1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAsia

Asia yaomboleza vifo vya tsunami miaka 20 baadae

26 Desemba 2024

Asia inakumbuka miaka 20 tangu janga kubwa la tsunami lilipogharimu maisha ya watu 220,000 na kuharibu maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi, likiwa moja ya majanga makubwa zaidi katika historia ya binadamu.

https://p.dw.com/p/4oZkx
Indonesia | Kumbukumbu ya miaka 20 ya Tsunami
Watu zaidi ya 160,000 walikufa nchini Indonesia kufuatia Tsunami iliyotikisa mataifa mengi ya ulimwenfu Desemba 26, 2024.Picha: AP

Mnamo Desemba 26, 2004, tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 9.1 karibu na ncha ya magharibi ya Indonesia lilisababisha mawimbi makubwa yaliyopiga pwani za nchi 14 kuanzia Indonesia hadi Somalia.

Kumbukumbu kwenye fukwe na ibada za kidini zitafanyika kote Asia, hususan Indonesia, Sri Lanka, India na Thailand, ambazo ndizo zilizoathirika zaidi. 

"Natumaini hatutawahi kupitia hali hiyo tena," alisema Nilawati, mama wa nyumbani wa Kiindonesia mwenye umri wa miaka 60, aliyepoteza mwanawe na mama yake katika janga hilo. 

Soma pia: Athari za Tsunami bado ni kubwa Indonesia

"Nimejifunza maumivu ya kupoteza mtoto, huzuni ambayo siwezi kueleza kwa maneno. Inaonekana kama ilitokea jana. Kila ninapokumbushwa, nahisi kama damu yote inanitoka mwilini." 

Waathirika wa mawimbi yaliyofikia urefu wa hadi mita 30 (futi 98) walijumuisha watalii wengi wa kigeni waliokuwa wakisherehekea Krismasi kwenye fukwe za eneo hilo, jambo lililofanya janga hilo kuhisiwa kote ulimwenguni. 

Thailand Khao Lak| Miaka 20 tangu janga la Tsunami
Bango lililoko kwenye mlango wa Hifadhi ya Kumbukumbu ya Tsunami ya Ban Nam Khem katika eneo la Khao Lak, Thailand.Picha: Carola Frentzen/dpa/picture alliance

Ufafanuzi wa EM-DAT, hifadhidata inayotambulika kimataifa ya majanga, unasema jumla ya watu 226,408 walifariki kutokana na tsunami hiyo. 

Kuwepo kwa mtandao wa kisasa wa vituo vya ufuatiliaji sasa kumepunguza muda wa kutoa tahadhari. 

Indonesia ilipoteza watu zaidi ya 160,000, ikiwa ndiyo iliyoathirika zaidi. Katika mkoa wake wa magharibi wa Aceh, waombolezaji walikusanyika kwa dakika ya ukimya, kisha kutembelea kaburi la pamoja na kufanya sala ya kijumuiya katika msikiti mkuu wa mji mkuu wa mkoa huo, Banda Aceh. 

Janga hilo pia lilihitimisha mzozo wa muda mrefu wa wapiganaji wa kujitenga huko Aceh, ambapo mkataba wa amani ulifikiwa kati ya waasi na Jakarta chini ya mwaka mmoja baadaye. 

Indonesia Simeulue 2023 | Kuhifadhi tamaduni za mdomo "Smong" huko Aceh
Miaka 20 baada ya tetemeko la ardhi na tsunami ya Bahari ya Hindi tarehe 26 Desemba 2004, watu katika Mkoa wa Aceh nchini Indonesia wanafanya juhudi za kuhifadhi na kueneza tamaduni za mdomo za Smong zilizookoa maisha ya wengi kwenye Kisiwa cha Simeulue huko Aceh.Picha: Hidayatullah/DW

Nchini Sri Lanka, ambapo zaidi ya watu 35,000 walifariki, manusura na jamaa walikusanyika kuwakumbuka takriban waathiriwa 1,000 waliokufa wakati mawimbi yalipogonga treni ya abiria na kuiondoa kwenye reli.

Soma pia: UN: Watu 190,000 wanahitaji msaada wa haraka Indonesia

Waombolezaji walipanda treni iliyorekebishwa ya "Ocean Queen Express" na kuelekea Peraliya, mahali ambapo treni hiyo iliharibiwa, kilomita 90 kusini mwa Colombo. 

Ibada fupi ya kidini ilifanyika pamoja na jamaa za marehemu huku ibada za Kibudha, Kihindu, Kikristo na Kiislamu pia zikiandaliwa kuwakumbuka waathiriwa kote katika kisiwa hicho cha Asia Kusini. 

Nchini Thailand, ambako nusu ya watu zaidi ya 5,000 waliokufa walikuwa watalii wa kigeni, maombolezo yasiyo rasmi yalitarajiwa kufuatia hafla ya ukumbusho ya serikali. 

Indonesia: Hadithi kuhusu manusura wa Tsunami ya Aceh 2004 na maisha yao ya sasa.
Nainunis, mmoja wa manusura kutoka Aceh, Indonesia, sasa anafundisha dansi ya break kwa vijana, wavulana na wasichana, katika mkoa unaofuata sheria za Kiislamu.Picha: Privat

Katika hoteli moja ya mkoa wa Phang Nga, maonyesho ya tsunami, filamu ya maandishi na maelezo kutoka kwa mashirika ya serikali na UN kuhusu hatua za maandalizi na uvumilivu wa majanga zilipangwa kufanyika. 

Soma pia: Kumbukumbu ya miaka 10 tangu janga la Tsunami

Karibu watu 300 walifariki katika nchi ya mbali ya Somalia, zaidi ya 100 katika Visiwa vya Maldives, na kadhaa nchini Malaysia na Myanmar. 

"Watoto wangu, mke wangu, baba yangu, mama yangu, na ndugu zangu wote walisombwa na maji," alisema Baharuddin Zainun, mvuvi na manusura mwenye umri wa miaka 70 kutoka Indonesia. 

"Janga hilo hilo liliwakumba wengine pia. Sote tunahisi maumivu sawa."