Katiba, Bunge vyasimamishwa kwa muda Syria
12 Desemba 2024Obaida Arnaout, msemaji wa serikali ya mpito ya Syria amesema tume za mahakama na haki za binadamu zitaanzishwa ili kuichunguza katiba na kisha kutoa mapendekezo katika kipindi hiki cha mpito. Akizungumza katika makao makuu ya televisheni ya taifa inayodhibitiwa na waasi waliotwaa mamlaka, Arnaout meeleza kuwa mkutano kati ya mawaziri wa "serikali ya wokovu" na mawaziri wa zamani umepangwa kufanyika Jumanne ili kufanya mchakato wa kukabidhiana madaraka.
Ameongeza kuwa, serikali ya mpito itaanzisha utawala wa sheria baada ya miaka mingi ya unyanyasaji chini ya Rais aliyeondolewa madarakani Bashar al Assad. Zaidi ameahidi kwamba wale wote waliofanya uhalifu dhidi ya watu wa Syria watahukumiwa kulingana na sheria.
Serikali hiyo mpya imesema pia kwamba inataka kuwa na mahusiano mazuri na mataifa yote, na imezishukuru Misri, Iraq, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jordan, Bahrain, Oman na Italia kwa kuendelea na shughuli katika balozi zao mjini Damascus.
Blinken azungumza na Mfalme Abdullah wa Jordan kuhusu Syria
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken, amekutana na kufanya mazungumzo na Mfalme Abullah wa Jordan wakati serikali ya Rais Joe Biden anayemaliza muda wake ikishinikiza kuundwa kwa serikali jumuishi katika taifa jirani la Syria baada ya utawala wa Bashar Al Assad kuangushwa.
Baada ya mkutano huo, Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mathew Miller amesema katika mazungumzo hayo Blinken ametilia pia mkazo kuundwa kwa serikali inayowajibika na kuwawakilisha watu wote iltakayochaguliwa na raia wote wa Syria. Baada ya Jordan Blinken anaelekea Uturuki akitafuta kuungwa mkono kwa misingi ambayo Marekani inatumaini itaongoza hatua zinazofuata Syria.
Soma zaidi: Waziri Mkuu mpya wa mpito wa Syria Mohammad al-Bashir aahidi kuwatendea haki raia wote Syria
Nao viongozi wa kundi la mataifa saba yaliyostawi zaidi kiviwanda G7 wamesema wako tayari kuunga mkono kipindi cha mpito katika katika juhudi za kupata serikali ya kuaminika, inaowajumuisha watu wote bila kujali imani zao nchini Syria.
Katika kauli ya pamoja viongozi hao wametoa wito wa kulindwa kwa haki za binadamu na kusisitiza umuhimu wa kuuwajibisha utawala wa Assad kisheria kwa uhalifu iliyoufanya.
Wametoa wito pia kwa wanaotaka kuongoza nchihiyo wazuie kuanguka kwa taasisi za serikali na wahakikishe mazingira salama na kurejeshwa nyumbani bila kushurutishwa kwa wote waliolazimika kuikimbia nchi hiyo.