1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 kuijadili Syria, serikali yaahidi utawala wa sheria

13 Desemba 2024

Viongozi wa kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiuchumi duniani ya G7, watajumuika mchana wa leo ( 13.12.2024) kutafuta muongozo wa pamoja kwa serikali mpya ya Syria.

https://p.dw.com/p/4o69e
Italien | Treffen der G7-Außenminister
Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya G7Picha: Andreas Solaro/AFP via Getty Images

Viongozi wa kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiuchumi duniani ya G7, watajumuika mchana wa 13.12.2024 katika kutafuta muongozo wa pamoja kwa serikali mpya ya Syria, ambayo imeahidi kulinda utawala wa sheria baada ya miaka mingi ya dhuluma chini ya rais aliyepinduliwa Bashar al-Assad.

Assad aliikimbia Syria baada ya mashambulizi makali yaliyoongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) na washirika wake, ambayo yalimaliza ghafla miongo mitano ya utawala kandamizi wa ukoo wake.

Viongozi hao wa Kundi la Mataifa Saba ambayo pia yana nguvu za kidemokrasia, watafanya mkutano kwa njia ya mtandao wamesema wako tayari kuunga mkono kipindi cha mpito kwa kile wanachokisema kuundwa serikali "jumuishi na isiyo ya kidini" nchini Syria.

Mataifa ya G7 yataka kuwajibishwa kwa utawala wa Assad kwa tuhuma za uhalifu

Ingawa tayari walitoa wito wa kulindwa kwa haki za binadamu, zikiwemo za wanawake na walio wachache, huku wakisisitiza "umuhimu wa kuuwajibisha utawala wa Assad kwa uhalifu wake". Na wakisema watafanya kazi na kuunga mkono kikamilifu serikali ya Syria ambayo inaheshimu kanuni hizo.

Türkei | syrische Geflüchtete in Gaziantep - Erdbeben 2023
Watoto wakitembea katika kambi ya wakimbizi wa Syria nchini Uturuki iliyoanzishwa na shirika la misaada la Uturuki AFAD katika wilaya ya Islahiye ya Gaziantep Februari 15, 2023.Picha: OZAN KOSE/AFP

Katika ujumbe unaofafana na huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, akiwa ziarani nchini Uturuki, ametaka wahusika huko Syria kuchukua hatua zote zinazowezekana kulinda raia, ikiwa ni pamoja na wanachama wa makundi ya walio wachache.

Juhudi za kutafuta ushahidi wa maovu ya Assad nchini Syria

Ndani nchini Syria lengo kwa sasa ni kufichua siri za utawala wa Assad, na hasa mtandao wa vituo vya kizuizini na maeneo yanayoshukiwa kuwa ya mateso yaliyotawanyika katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa chini ya udhibiti wa serikali.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema wamekusanya orodha za siri za wahusika 4,000 wa uhalifu mkubwa nchini Syria tangu siku za mwanzo za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Na Wizara ya Sheria ya Marekani jana Alhamisi ilimfungulia mashtaka mkuu wa zamani wa Gereza Kuu la Damascus, Samir Ousman Alsheikh, kwa kuwatesa wapinzani wa Assad.

Vikosi vya Israel vinaendelea kusalia katika ukanda usio wa vita katika ardhi ya Syria

Katika hatua nyingine wizara ya ulinzi ya Israel imesema vikosi vyake vilivyoiingia katika eneo la Syria la milima ya Herman na Golan yaendelee kusalia katika maeneo hayo katika msimu huu wa baridi kwa lengo la kujilinda kimkakati, hatua ambayo imezusha ukosoaji wa kimataifa. Israel inasema eneo hilo la ukanda usio wa kivita ni muhimu kwa kuweza kudhibiti usalama wao kwa kuwa wanaweza kuliona eneo kubwa la Syria na Lebanon.

Soma zaidi: Blinken asema raia wa Syria wanahitaji kulindwa

Kuporomoka kwa utawala wa Assad kunafunga enzi ambayo watu wanaoshukiwa kuwa wapinzani walifungwa au kuuawa, na kuhitimisha karibu miaka 14 ya vita vilivyoua zaidi ya watu 500,000 na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.

Vyanzo: AFP/DPA