HTS kujivunja na kujiunga na jeshi la Syria
18 Desemba 2024Mkuu wa kijeshi wa kundi la HTS, Muhraf Abu Qasra, maarufu kama Abu Hassan al-Hamawi, aliliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumanne (Disemba 17) kwamba kundi hilo litalivunja tawi lake la kijeshi na kujiunga na jeshi rasmi la serikali mara tu mipango itakapokuwa tayari.
Abu Qasra alisema pia kwamba maeneo yanayoshikiliwa na waasi wa Kikurdi yatakuwa chini ya utawala mmoja wa serikali kuu ya Syria na kwamba kundi lake linapingana moja kwa moja na wazo la kuifanya Syria kuwa nchi ya majimbo yenye tawala zake za ndani.
Soma zaidi: Baada ya Syria, je, utawala wa Iran utafuata na kuanguka?
"Katu Syria haitagawanywa vipande vipande. Itaendelea kuwa Syria moja." Alisisitiza.
Kauli kama hiyo ilirejelewa na mkuu wa HTS, Muhammad Al-Joulani, ambaye kwenye mkutano wake na waandishi wa habari usiku wa kuamkia Jumatano alisema kwamba Syria ingeliongozwa na katiba mpya ambayo haina tafauti sana na ile ambayo Wasyria wameizowea.
Wanajeshi wa Israel ndani ya Syria
Kuhusu suala la Israel kuendelea kubakisha wanajeshi wake ndani ya ardhi ya Syria, Joulani alisema hoja ya Tel Aviv kwamba iliingia Syria kwa sababu ya wanamgambo wa kundi la Hizbullah la Lebanon na washirika wao wa Iran haina uzito wowote "kwa kuwa sasa hakuna tena wapiganaji wa Iran wala Hizbullah waliobakia."
Badala yake, kiongozi huyo wa HTS, alitowa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuitaka Israel iheshimu sheria za kimataifa na iwaondowe wanajeshi wake kwenye ardhi ya Syria, akihakikisha kwamba kamwe nchi yake "haitatumika kuishambulia Israel wala taifa jengine lolote."
Soma zaidi: Netanyahu: Wanajeshi watabakia eneo la ukanda salama na Syria
Kauli ya uongozi mpya wa Syria inakuja wakati Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akitembelea Mlima Hermon, ndani ya Syria, eneo ambalo jeshi lake lililikamata mwezi huu, mara tu baada ya utawala wa Assad kuporomoka.
Netanyahu akiwa pamoja na waziri wake wa Ulinzi, Israel Katz, na maafisa wa ngazi za juu wa usalama walilitembelea eneo hilo kwa mara ya kwanza tangu walipolivamia takribani wiki mbili zilizopita.
Soma zaidi: Baraza la Usalama: Mchakato wa kisiasa Syria uwe jumuishi
Kwa upande wake, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetowa wito wa kuanzishwa kwa mchakato wa kisiasa unaowajumuisha na kuongozwa na Wasyria wenyewe.
Kwenye tamko la Jumanne, Baraza hilo la Usalama lilisema kwamba mchakato huo "unapaswa kuendana na matazamio halali ya Wasyria wote, kuwalinda na kuwawezesha kuishi kwa usalama, kwa uhuru na kidemokrasia kuelekea kwenye mustakabali mpya."
/AFP, Reuters