Jordan kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya mageuzi ya Syria
14 Desemba 2024Mkutano huo unafanyika siku moja tu, baada ya sherehe mjini Damascus na kote nchini Syria kufurahia kuangushwa kwa mtawala wa kiimla rais Bashar al-Assad. Kuanguka kwa Assad pia kumesababisha maendeleo ya haraka ya kidiplomasia, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa miongoni mwa wajumbe wanaotarajiwa kuijadili Syria leo hii katika mji wa Aqaba nchini Jordan. Mwanadiplomasia wa Qatar amesema wajumbe kutoka katika taifa la Ghuba watazuru Syriakesho Jumapili kukutana na maafisa wa serikali ya mpito na kujadili msaada na kufunguliwa tena kwa ubalozi wao. Na kadhalika Uturuki ikitangaza kuwa itaufungua tena ubalozi wake mjini Damascus, uliofungwa tangu mwaka 2012.Assad ameikimbia Syria, na kuhitimisha enzi ambayo watu wanaoshukiwa kuwa wapinzani walifungwa au kuuawa, na kumaliza karibu miaka 14 ya vita vilivyoua zaidi ya watu 500,000 na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.