Jumuiya ya kimataifa haielewi athari za mgogoro wa Sudan?
17 Desemba 2024Afisa huyo wa ngazi ya juu ambaye ni Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR nchini Sudan, Mamadou Dian Balde, amesema juhudi za kidiplomasia "hazilingani na mahitaji".
Balde ameeleza kwenye mahojiano katika makao makuu ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, kwamba hadhani kama dunia inatambua uzito wa mgogoro wa Sudan, na athari zake.
Amesema wakati mwaka unapokaribia kumalizika, UNHCR na washirika wake wamepokea asilimia 30 tu ya dola bilioni 1.5 walizoomba kwa ajili ya kushughulikia mpango wa kikanda wa kuwasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Sudan katika mwaka huu wa 2024.
Vita kati ya Jeshi la serikali na vikosi vya RSF, vilivyozuka katikati ya Aprili mwaka 2023, vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Soma Pia: Wapiganaji wa RSF watuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita Sudan
Mzozo huo pia umewalazimisha watu wapatao milioni 12 kuyakimbia makazi yao, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu katika kumbukumbu za hivi karibuni.
UNHCR imesema katika miezi 20 ya vita, watu milioni 3.2 tayari wameikimbia Sudan, huku wengine zaidi ya milioni 8.6 wakilazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani ya nchi hiyo yenye vita.
Shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa limesema vilevile kuna zaidi ya wakimbizi 264,000 kutoka nchi nyingine ambao walikimbia nchi zao kutokana na mizozo na bado wamesalia ndani ya Sudan.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Shirika la kuwahudumia wakimbizi nchini Sudan, Mamadou Dian Balde amesema pande zote mbili katika mzozo zinapaswa kulaumiwa kwa kuitumia njaa kama silaha ya vita, kuzuia au kupora misaada ya kibinadamu na kwa kufanya unyanyasaji mkubwa, ikiwa ni pamoja na mateso na unyanyasaji wa kijinsia.
Balde pia amelaumu dhana potofu kwamba vita vinavyoendelea nchini Sudan ni mgogoro wa kikanda, amesisitiza kwamba vita hivyo hakika vimesababisha tatizo la kimataifa.
Amefahamisha kwamba watu wengi wanaokimbia mzozo huo wa nchini Sudan wamesafiri nje na kuingia katika nchi jirani, huku watu wapatao 60,000 wakiwa tayari wamefika nchini Uganda na katika upande wa kusini mwa nchi Jirani ya Sudan Kusini. Amesema ni swala la kufikiria tu ni watu wangapi watakuja kwenye bara la Ulaya ikiwa hali hii itaendelea.
Msemaji wa UNHCR, Olga Sarrado amesema shirika hilo limezidi kuwa na wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya watu wanaovuka kwenye mpaka wa kusini kuelekea Sudan Kusini.
Amesema wakati wastani wa kila siku hadi hivi majuzi ulikuwa karibu watu 800 wanaovuka mpaka huo kwa siku, katika kipindi cha wiki mbili idadi ya watu 40,000 walikuwa wamevuka mpaka huo wakiwa wanakimbia kutoka Sudan na kuingia Sudan Kusini. Watu hao wamehifadhiwa katika kambi za wakimbizi.
Soma Pia: UN yatoa wito wa kushughulikia mzozo wa Sudan
Akiangazia ukubwa wa mgogoro huo Mamadou Dian Balde, ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mataifa yenye ushawishi kwa pande zinazohusika na mzozo huo kuzishawishi juu ya kuvimaliza vita hivyo.
Chanzo: AFP