1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la G7 lasema liko tayari kuisaidia Syria

12 Desemba 2024

Viongozi wa kundi la G7, wamesema wako tayari kusaidia mchakato wa kipindi cha mpito nchini Syria, utakaoongozwa kwa utawala wa kuaminika, unaowajumuisha wote na usio wa kidini.

https://p.dw.com/p/4o4iH
Wasyria baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad
Wasyria baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad.Picha: OMAR HAJ KADOUR/AFP/Getty Images

Taarifa ya G7 iliyotolewa leo, imeeleza kuwa mabadiliko ya kisiasa baada ya kumalizika utawala wa kimabavu wa Bashar al-Assad, unapaswa kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu kwa wote, ikiwemo haki za wanawake, kuwalinda Wasyria wote, ikiwa ni pamoja na dini na makabila madomo, uwazi na uwajibikaji.

Viongozi hao pia wamezitaka pande zote kulinda uadilifu wa eneo la Syria na umoja wa kitaifa, na kuheshimu uhuru na mamlaka yake.

Wakati huo huo, serikali mpya ya Syria imesema katiba na bunge la nchi hiyo vitasitishwa kwa muda wa miezi mitatu, wakati wa kipindi cha mpito.