Viongozi wa dunia wapongeza Assad kuondolewa madarakani
8 Desemba 2024Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema kwa sasa Syria haitakiwi kuanguka katika mikono ya makundi mengine yaliyo na itikadi kali. Amehimiza ulinzi kamili wa makundi ya kidini na makabila ya wachache kama ya Wakurdi na Wakristo.
Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Angela Rayner, amesema kile kinachohitajika kwa sasa ni uthabiti wa kikanda akisema udikteta na ugaidi umesababisha madhila makubwa kwa watu wa Syria.
Waasi wa Syria waingia Damascus, wasema Assad amekimbia
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Geir Pedersen pia amezungumzia hali ya Syria na kusema ukurasa mpya umefunguliwa nchini humo na anatumai utakuwa wa amani, maridhiano, uadilifu na unaowajumuisha Wasyria wote.
Rais wa Marekani Joe Biden kupitia msemaji wa usalama wa kitaifa Sean Savett, amesema Marekani inafuatilia matukio ya Syria kwa karibu, huku Ufaransa ikisema itaendelea kusimamia usalama wa kanda nzima na kuitakia Syria amani umoja na uhuru.
China pia imesema inafuatilia kwa karibu hali nchini Syria.