Saudi Arabia yaanza kampeni ya kupeleka misaada Syria
1 Januari 2025Kampeni hiyo ya kutumia njia ya anga kufikisha misaada, imeanzishwa na kituo cha kutoa misaada ya kibinadamu KSrelief, ikilenga kuwaondolewa hali ngumu inayowakumba raia wa Syria.
Mataifa kadhaa yakiwemo ya Umoja wa Ulaya pamoja na Ukraine pia yametangaza kuipa Syria misaada zaidi, wakati Umoja wa Mataifa ukieleza kuwa, watu saba kati ya kumi wanahitaji msaada nchini humo.
Soma pia: Syria yamteua kamanda wa HTS kuwa waziri wa ulinzi
Shirika rasmi la habari la Saudi Arabia SPA limeripoti kuwa "daraja la anga" la utawala mjini Riyadh litafuatiwa na kampeni nyingine ya kutumia njia za ardhi kufikisha misaada katika siku zijazo.
Syria imeharibiwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 13 pamoja na vikwazo vya mataifa ya Magharibi vilivyoilenga serikali ya rais aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad.