Syria yamteua kamanda wa HTS kuwa waziri wa ulinzi
31 Desemba 2024Abu Qasra, ambaye hapo awali alikuwa mtaalamu wa kilimo na kiongozi wa kijeshi wa kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), alitoa mchango muhimu katika kampeni iliyomuondoa madarakani Bashar al-Assad. Tangazo hilo lilitolewa kupitia shirika rasmi la habari SANA.
Abu Qasra, mwenye umri wa miaka 41, ambaye awali alijulikana kwa jina la vita la Abu Hassan al-Hamawi, linaloashiria mkoa wake anakotokea wa Hama, alisisitiza katika mahojiano ya hivi karibuni juu ya umuhimu wa kuunganisha vikundi vyote vya kijeshi, ikiwa ni pamoja na HTS, katika vikosi vya kitaifa vya Syria.
Uongozi wake umejikita katika juhudi za kuimarisha hali ya kijeshi iliyovurugika huku akikabiliana na vitisho vya usalama kama mashambulizi ya mara kwa mara ya Israeli kwenye ardhi ya Syria.
Serikali ya mpito, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa mpito Mohammad al-Bashir, inafanya kazi ya kuimarisha mamlaka yake, ikiwa ni pamoja na mipango ya kupanua usimamizi wake hadi maeneo yanayoshikiliwa na Wakurdi.
Soma pia: Polisi 14 wa Syria wauawa katika shambulio ka kuvizia Tartus
Hata hivyo, uongozi mpya unasalia kuwa na tahadhari kuhusu kuingia kwenye migogoro mipya, ukizingatia kipaumbele cha kuleta utulivu kwa Syria iliyoharibiwa na vita.
Mwanamke awa gavana wa Benki Kuu
Katika hatua ya kihistoria, serikali mpya Syria imemteua Dkt. Maysa Sabreen kuwa gavana wa mpito wa Benki Kuu ya Syria. Hii ni mara ya kwanza mwanamke kushika wadhifa huu katika historia ya nchi hiyo.
Sabreen, mtaalamu wa masuala ya benki, hapo awali alihudumu kama naibu gavana wa kwanza wa benki hiyo tangu mwaka 2018 na alishikilia nafasi muhimu katika bodi mbalimbali za kifedha na udhibiti.
Soma pia: Watawala wapya Syria wateua waziri wao wa mambo ya nje
Uteuzi wa Sabreen unakuja wakati muhimu ambapo Syria inakabiliana na athari za vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe na kuondolewa kwa Bashar al-Assad madarakani.
Sarafu ya kitaifa imepoteza thamani yake kwa asilimia 90 tangu mwaka 2011. Sabreen anatarajiwa kukabiliana na changamoto hizi huku akiongoza juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.
Gavana wa zamani, Mohammed Issam Hazime, alihudumu chini ya utawala wa Assad hadi kuondolewa kwake mapema mwezi huu. Uongozi wa Sabreen unaashiria enzi mpya kwa taasisi za kifedha za Syria katikati ya mabadiliko mapana ya kisiasa.
Wakimbizi waongeza kasi ya kurudi nyumbani
Zaidi ya wakimbizi wa Syria 35,000 wamerudi kutoka Uturuki kwenda Syria kufuatia kuondolewa kwa Bashar al-Assad madarakani mapema mwezi huu, kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya.
Ongezeko hili la haraka la kurejea kwa wakimbizi ni sawa na wastani wa miezi mitatu kwa muda wa wiki chache tu, jambo linaloonyesha athari za mabadiliko ya hivi karibuni ya kisiasa.
Uturuki, ambayo imekuwa mwenyeji wa idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria, ina jumla ya wakimbizi takriban milioni 2.9, wakiwemo karibu watoto milioni moja waliozaliwa nchini humo.
Hata hivyo, uhasama unaoongezeka dhidi ya wakimbizi nchini Uturuki umechochea wito wa kurudi kwao nyumbani.
Kuanguka kwa utawala wa Assad kumesherehekewa na Wasyria walioko uhamishoni kote duniani, hasa kutokana na kuachiliwa kwa maelfu ya wafungwa kutoka magereza mabaya ya utawala huo.
Ingawa kuna maendeleo chanya, serikali mpya ya mpito inakabiliwa na changamoto kubwa za kuhakikisha amani na mshikamano katika Syria iliyogawanyika.
Kwa ahadi za kuheshimu makundi yote ya kidini na kidemografia, uongozi wa mpito unatarajia kuleta mazingira yatakayochochea kurejea kwa hiari na maridhiano.
Wanasheria wataka uchaguzi huru wa chama chao
Wanasheria wa Syria wamezindua ombi la mtandaoni wakitaka uchaguzi huru wa chama cha wanasheria baada ya watawala wapya kuteua baraza la muda la kusimamia chama hicho.
Ombi hilo linasisitiza kuwa chama hicho hakipaswi kuwa chini ya mamlaka yoyote na linataka uchaguzi wa haraka wa kidemokrasia ili kurejesha uhuru na jukumu lake la kihistoria la kulinda haki za watu na jamii.
Soma pia: Mjumbe wa UN Syria ataka vikwazo viondolewe baada ya Assad
Ombi hilo, lililosainiwa na wanasheria kutoka Damascus, Homs, na Hama, linaonya dhidi ya kuteua viongozi wasiochaguliwa, likisema kuwa hatua hiyo itadumisha ukandamizaji wa haki.
Wanasheria hao wanapendekeza uchaguzi wa huru kwa chama na matawi yake kote nchini bila kuchelewa ili kuhakikisha uwajibikaji na demokrasia.
Chama cha wanasheria kilikuwa mstari wa mbele katika kupinga ukandamizaji mwanzoni mwa miaka ya 1980 kabla ya kudhibitiwa na utawala uliopita. Sasa, wanasheria wanataka kukirejesha kama taasisi huru inayoweza kuchangia katika kipindi hiki muhimu cha mpito.
Mamlaka mpya za Syria zimesimamisha katiba na bunge kwa muda wa miezi mitatu, na kiongozi Ahmed al-Sharaa alisema uchaguzi wa kitaifa unaweza kuchukua hadi miaka minne, huku uandaji wa katiba mpya ukitarajiwa kuchukua miaka miwili au mitatu.