Urusi yapuuza sheria ya kudhibiti silaha
18 Desemba 2024Mkuu wa majeshi Urusi Valery Gerasimov, amesema nchi yake inatizama sheria ya kudhibiti zana za nyuklia zilizotengenezwa enzi za Vita Baridi, kupitwa na wakati kutokana na ukosefu wa uaminifu kati ya Urusi na nchi za Magharibi.
Gerasimov ameilaumu Marekani kwa kuchochea machafuko kote ulimwenguni na kuhujumu sheria za kudhibiti silaha hatari. Amesema kwa kujibu hilo, Urusi itaunda ushirikiano na China, India, Iran, Korea Kaskazini na Venezuela.
"Mada kuhusu udhibiti wa silaha imepitwa na wakati, kwa kuwa kwa kurejea kwa kiwango cha chini cha kuaminiana, utekelezaji wake ni vigumu kwa sababu ya undumakuwili wa nchi za Magharibi. Bila uaminifu ni vigumu kuweka mfumo thabiti wa udhibiti kwa pande zote," amesema Valery Gerasimov.
Hayo yamejiri wakati Urusi ikiishutumu Ukraine kwa kutumia mara kwa mara silaha za kemikali aina ya Phosphorus mnamo mwezi Septemba.
Soma pia: Urusi yadai kumzuilia mshukiwa aliyemuua Igor Kirillov
Maria Zakharova, msemaji wa wizara ya Ulinzi ya Urusi amesema vyombo vya usalama vina ushahidi kwamba Ukraine ilitumia zana hizo, lakini bila ya kutoa maelezo.
Ukraine yakanusha kutumia silaha za kemikali
Heorhii Tykhyi, ambaye ni msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje wa Ukraine amesema madai ya Urusi si kweli. Ameongeza kuwa Ukraine inaendelea kuwa mshirika wa kuaminika kimataifa kutoeneza silaha za maangamizi makubwa, na inakubaliana kwa uaminifu na sheria na masharti ya kimataifa kuhusu hilo.
Urusi pia imeishutumu Ukraine kwa kile ilichokiita kufanya "shambulizi la kigaidi” lililomuua jenerali wake mkuu wa ulinzi wa nyuklia pamoja na msaidizi wake mjini Moscow siku ya Jumanne.
Soma pia: Urusi: Jenerali wa ulinzi wa nyuklia Igor Kirillov auawa
Akizungumza na waandishi Habari na kwa mara ya kwanza kuhusu shambulizi lililomuua Igor Kirillov, msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov amesema ni wazi sasa ni nani aliamuru shambulizi la kigaiudi dhidi yao. Kulingana na Peskov, kwa mara nyingine tukio hilo linathibitisha kwamba utawala wa Ukraine haichelei kutumia mbinu za kigaidi.
Urusi yasema imekamata vijiji viwili Donetsk
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema imekamata vijiji viwili vipya katika jimbo la Donetsk mashariki mwa Ukraine
Katika taarifa yake ya kila siku kuhusu uvamizi wake nchini Ukraine, wizara hiyo imesema vikosi vyake vimekomboa kijiji cha Stairi Terny na Trudove ambavyo viko karibu na mji wa Kurakhove ambao unaonekana uko karibu pia kuanguka mikononi mwa Urusi.
Soma pia: Mawaziri wa EU wasaini vikwazo vipya dhidi ya Russia
Kwa miezi sasa, Urusi imekuwa ikiendelea kusonga mbele katika uwanja wa mapambano mashariki mwa Ukraine huku vikosi vyake vikiwazidi idadi na nguvu wanajeshi wa Ukraine katika eneo hilo.
Kurakhove ni mji wa kimkakati wa viwanda kwenye ukingo wa hifadhi ambayo Moscow inajaribu kukamata.
(AFPE, RTRE, EBU)