Viongozi wa EU wasema wataendelea kuiunga mkono Ukraine
19 Desemba 2024Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamemualika Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kushiriki katika mkutano wao ili kumhakikishia uungaji mkono wao wa dhati kwa taifa lake kwa muda wote utakaohitajika. Hii ni kwa mujibu wa rasimu ya mkutano huo. Hata hivyo, Donald Trump ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka vita kati ya Urusi na Ukraine kusitishwa mara moja. Awali Trump alisisitiza kuwa Zelensky lazima awe tayari kufikia makubaliano ya amani na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ingawa hakufafanua ikiwa hilo linahusisha Kiev kuachia baadhi ya maeneo yake kwa Moscow kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza vita hivyo.
Rais Zelensky aomba washirika wa Ulaya kuwasaidia kwa umoja
Kwa sasa, Urusi inashikilia karibu humusi moja ya maeneo ya Ukraine na inaendelea kusonga mbele katika maeneo ya mashariki mwa taifa hilo. Katika mkutano huo, viongozi wa Umoja wa Ulaya pia watajadili kwa kina uhusiano kati ya Umoja huo na Marekani, hasa vita vya kibiashara vilivyotangazwa na Trump.
Rais huyo wa zamani wa Marekani amedai kuwa Ulaya haitoshi kununua bidhaa za Marekani, na ameahidi ushuru mkubwa kwa mataifa ya Ulaya, kufuatia hatua kama hizo dhidi ya Canada, Mexico, na China. Umoja wa Ulaya una hofu kuwa huenda nao usiepuke hatua hiyo.
Uingereza yatoa msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine
Wakati huohuo, Uingereza ilitangaza msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine wa dola milioni 286 kwa mwaka 2025, ukijumuisha droni, maboti, na mifumo ya ulinzi wa anga. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey, alifanya ziara mjini Kiev na kukutana na mwenzake wa Ukraine, Rustem Umerov, ambapo aliahidi kuimarisha msaada wa Uingereza kwa Ukraine. Healey alisema kuwa miaka mitatu baada ya Urusi kuvamia Ukraine, taifa hilo bado linaendelea kupambana na mipango ya Putin.
Ukraine yasema wanajeshi wengi wa Korea Kaskazini wameuawa Kursk
Katika mkutano huo wa Umoja wa Ulaya, viongozi wanatarajiwa kuidhinisha msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo zaidi kwa wanajeshi wa taifa hilo. Aidha, viongozi hao wamesisitiza kuwa hakuna suluhisho lolote la kumaliza vita hivyo litakalofikiwa bila ushiriki wa Ukraine, hasa wakati huu ambapo Donald Trump anatarajiwa kuapishwa rasmi kama Rais wa Marekani mnamo Januari 20.
Huku hayo yakiarifiwa Mbunge wa Korea Kusini Lee Seong-kweun amwaambia waandishi habari kuwa wanajeshi 100 wa Korea Kaskazini waliotumwa kulisaidia jeshi la Urusi katika vita vyake na Ukraine wameuwawa tangu walipojiingiza katika mapambano hayo mwezi Disemba. Inadaiwa kuwa Pyongyang imetuma maelfu ya wanajeshi kulisaidia jeshi la Urusi katika eneo la mpakani la Kursk linalodhibitiwa kwa sasa na Ukraine.
afp,ap,reuters