1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Zelensky aomba washirika wa Ulaya kuwasaidia kwa umoja

19 Desemba 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaomba washirika wake wa Ulaya kushikamana wanapolisaidia taifa hilo kwa ajili ya usalama badala ya kugawanyika.

https://p.dw.com/p/4oKqw
Rais Zelensky akiwa na Mark Rutte, katibu Mkuu wa NATO
rais Volodymyr Zelensky akizungumza na katibu Mkuu wa Nato Mark Rutte mjini Kyiv, Oktoba 03, 2024Picha: Ukraine Presidency/Bestimage/IMAGO/

Kiongozi huyo wa Ukraine alikuwa katika makazi rasmi ya Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte kwa ajili ya mkutano wa kujadili mustakabali wa Ukraine, wakati Donald Trump anakaribia kurejea madarakani.

Kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Rutte, walijadiliana pia kuhusu dhamana ya usalama nchini Ukraine, ikiwa kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, vyanzo vimeliambia shirika la habari la DPA.

Suala jingine muhimu lilikuwa ni namna ambavyo usitishwaji huo utakavyofuatiliwa, huku kukiwa na pendekezo moja kubwa la kuwa na kikosi cha kimataifa cha kulinda amani.

Zelensky alitarajiwa kukutana na Rutte, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uigereza David Lammy, Rais wa Poland Andrzej Duda na wanachama wakubwa wa Ulaya kwenye jumuiya ya NATO.

Soma pia: Viongozi wa mataifa ya Ulaya na NATO kuijadili Ukraine

Marekani New York | Zelensky akutana na Trump
rais Donald Trump akipeana mkono na Rais Volodymyr Zelensky alipozuru Marekani Septemba 27m 2024Picha: Alex Kent/Getty Images

Kuna wasiwasi barani Ulaya kwamba serikali ya Trump huenda itajaribu kuishinikiza Ukraine kuingia kwenye makubaliano na Urusi, pengine kwa kutishia kusitisha misaada ya kijeshi ikiwa itakataa kuanza mazungumzo ya amani.

Rais Zelensky azungumza tena na Macron kuhusu jeshi la kimataifa

Katikati ya minong'ono kuhusiana na mustakabali wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Urusi, Rutte amesema anataka kuzungumza na Zelenky kuhusu namna watakavyoweza kuhakikisha taifa hilo linakuwa katika nafasi nzuri zaidi, wakati watakapoamua kuanza mazungumzo hayo ya amani.

Soma pia:Trump asema Zelensky ana nia ya kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine

Mbali na mkutano huo wa Brussels, Rais Zelenksy amesema amekuwa na duru mpya ya mazungumzo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusiana na pendekezo la karibuni la kupeleka wanajeshi nchini Ukraine, kama njia ya kuisaidia kufikia amani thabiti. 

Ameandika kwenye mtandao wa X kwamba wanaendelea kushughulikia mpango wa Rais Macron unaohusiana na kupeleka wanajeshi nchini humo watakaosaidia kuleta utulivu katika kipindi cha mpito kuelekea kurejesha amani. Macron alitoa pendekezo hilo kwa mara ya kwanza mwezi Februari.

Andrei Belousov azuru Korea Kaskazini
Mawaziri wa Ulinzi wa korea Kaskazini No Kwang-chol (kulia) na mwenzake wa Urusi Andrei Belousov(kushoto) baada ya mazungumzo mjini Pyongyang Novemba 29, 2024Picha: Russian Defence Ministry/AFP

Korea Kaskazini yalaani tamko la Marekani kuhusu uhusiano wake na Urusi

Na huko mjini Seoul taarifa zimesema, Korea Kaskazini mapema leo imesema muungano wa kijeshi na Urusi unaonyesha mafanikio makubwa katika kuizuia Marekani na vikosi ilivyoviita "vibaraka wake" huku ikikosoa vikali matamshi ya karibuni ya Washington na washirika wake dhidi ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Pyongyang na Moscow.  

Korea Kaskazini hata hivyo haikuzungumzia chochote kuhusiana na kujiingiza kwenye vita vya Ukraine ama madai ya vifo na wanajeshi wake kujeruhiwa katika mapambano kwenye mkoa wa Kursk, na badala yake ililaani taarifa iliyotolewa na Marekani na mataifa tisa ya Ulaya siku ya Jumatatu, ikiita iliyojaa upotoshaji na kutia doa msingi wa ushirika wa kawaida kati ya taifa hilo na Urusi.

Tukigeukia uwanja wa vita, Gavana wa mkoa wa Rostov Yuri Slyusar amesema mifumo ya jeshi la anga la Urusi imezuia shambulizi la Ukraine ambayo ilivurumisha makombora 10 kuelekea kwenye mkoa huo ulioko kusini mwa Urusi jana Jumatano.

Afisa wa Ukraine amesema shambulizi hilo liliulenga mtambo wa nyuklia unaosambaza mafuta ya roketi kwenye vikosi vya Urusi.

Hata hivyo hakukutipotiwa majeruhi wala vifo.