Watawala wa Syria waanzisha operesheni kwenye ngome ya Assad
26 Desemba 2024Shirika la habari la serikali - SANA limesema vikosi vya usalama vilifanya msako dhidi ya wapiganaji wanaomuunga mkono Assad katika mkoa wa magharibi wa Tartus, na kuwauwa wanamgambo kadhaa. Shirika linalofuatilia hali nchini Syria, Syrian Observatory for Human Rights limesema wapiganaji watatu wanaohusishwa na serikali ya Assad waliuawa kwenye operesheni hiyo.
Imefanywa siku moja baada ya maafisa 14 wa polisi wa serikali ya mpito na wapiganaji watatu kuuawa katika makabiliano yaliyozuka kwenye mkoa huo. Yalitokea wakati vikosi vya ndani vilijaribu kumkamata afisa mmoja wa utawala wa Assad.
Shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Uingereza limesema Mohammed Kanjo Hassan, alikuwa afisa wa sheria wa kijeshi aliyetoa hukumu za kifo na hukumu za kiholela dhidi ya maelfu ya wafungwa katika gereza kuu la Saydnaya. Gereza hilo, eneo kulikofanywa mauaji ya kiholela, mateso na watu kutekwa, lilidhihirisha ukatili uliofanywa dhidi ya wapinzani wa Assad.