1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kusitisha mapigano ya Gaza yashika kasi Cairo

18 Desemba 2024

Maafisa kwenye mazungumzo hayo wanashinikiza hatua za kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza. Marekani na Israel zimesema zina matumaini makubwa kuhusu kufikiwa makubaliano hayo

https://p.dw.com/p/4oI8x
Mashariki ya Kati Makubaliano ya kusimamisha vita | Vita katika Ukanda wa Gaza
Mgogoro wa Mashariki ya KatiPicha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Makubaliano ya kusimamisha vita vinavyoendelea kwa muda wa miezi 14 sasa katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko yanaweza kutiwa saini katika siku mbili tatu zijazo kutokana na kupiga hatua nzuri mazungumzo yanayoendela mjini Cairo, hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vya habari kuhusu mkutano huo.

Wajumbe wa Marekani, wamejiunga pamoja na wapatanishi kutoka Misri na Qatar, wamekuwa wanafanya juhudi kubwa katika siku za hivi karibuni ili kufikia makubaliano katika mazungumzo hayo kabla ya Rais Joe Biden kuondoka madarakani mwezi ujao.

Baraza la Usalama la Kitaifa | John Kirby | Ikulu ya Marerkani
Mratibu wa Baraza la Usalama la Kitaifa na Mawasiliano ya Kimkakati wa Ikulu ya Marekani, John KirbyPicha: Ken Cedeno/UPI/newscom/picture alliance

Mratibu wa Baraza la Usalama la Kitaifa na Mawasiliano ya Kimkakati wa Ikulu ya Marekani, John Kirby, amesema katika mahojiano na shirika la Habari la Fox News kwamba wao wanaamini na pia wanaamini wanachokisema Waisraeli kwamba makubaliano yanakaribia kufikiwa ingawa Marekani imesema inafuatilia matumaini hayo kwa uangalifu.

Soma Zaidi: Marekani yaona ishara ya makubaliano ya Gaza

Kirby alipoulizwa kwamba huu ni mwezi Desemba Je, makubaliano hayo yanaweza kufikiwa kabla yasikukuu ya Krismasi? alijibu kwamba Marekani inajaribu kila linalowezekana na inatilia maanani kwamba mateka wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza wanahitaji kurudi nyumbani kuungana na familia zao.

Wakati huo huo mkurugenzi wa shirika la kijajsusi la Marekani, (CIA) Bill Burn, yupo mjini Doha kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani katika juhudi za kuziba mapengo yaliyosalia kati ya Israel na Hamas. Wawili hao watajadili maendeleo kuelekea kusitishwa vita vya Gaza na mpango wa kuwaachilia huru mateka.

Wakati hayo yakiendelea shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza limesema mashambulizi ya Israel katika eneo hilo yamesababisha vifo vya wapalestina waliokimbia makazi yao. Watu hao walikuwa wamejihifadhi kwenye nyumba moja.

Msemaji wa shirika hilo la ulinzi wa raia Mahmud Bassal, amesema Wapalestina hao 10 waliuawa wakati wa mashambulizi ya Israel ya leo alfajiri katika eneo la Beit Lahia, kaskazini mwa Gaza.

Soma Zaidi: Israel yashambulia Kaskazini mwa Gaza na kuua watu 20

Na familia za Wapalestina huko nchini Marekani zimefungua kesi ya kuishtaki Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kutokana na Marekani kuliunga mkono jeshi la Israel katika vita vyake huko Gaza ambavyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na pia kusababisha mgogoro wa kibinadamu kulingana na jalada la mahakama kuhusu kesi hiyo iliyowasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Columbia.

DW-Video | Columbia, Marekani maandamano ya kupinga mgogoro wa Mashariki ya Kati
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Columbia waandamana kupinga mgogoro wa Mashariki ya KatiPicha: Aya Ibrahim/DW

Katika kesi hiyo Wizara ya Mambo ya Nje chini ya Waziri Antony Blinken imekiuka kwa makusudi sheria ya haki za binadamu ya Marekani kwa kuendelea kufadhili na kuyasaidia majeshi ya Israel yanayotuhumiwa wa ukatili katika Ukanda wa Gaza na katika Ukingo wa Magharibi.

Vyanzo: RTRE/AP